Katika siku za hivi karibuni ripoti zinaeleza kuwa kumetokea mlipuko
wa ugonjwa wa homa ya dengue katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki
ambapo nchini Tanzania Wizara ya Afya imetangaza kuwa watu karibu 400
wamekwishagunduliwa kuugua ugonjwa huo. Homa ya dengue si ugonjwa
uliozoeleka kwa wengi na kwa ajili hiyo kipindi chetu cha leo
kitayajadili maradhi hayo, ili kuwapa watu ufahamu wa dalili za ugonjwa
huo, maambukizo yake na namna ya kujikinga. Natumaini mtajumuika nami
hadi mwisho wa kipindi hiki.
Dengue Fever yaani homa ya dengue inaendelea kuenea kwa kasi nchini
Tanzania baada ya takwimu kuonesha kuwa, kuanzia mwezi Januari mwaka huu
hadi sasa mkoani Dar es Salaam pekee watu 376 wamembukizwa ugonjwa
huo.
Mtaalamu wa Ufuatiliaji wa Magonjwa wa Wizara ya Afya ya Tanzania
Dakta Janeth Mugamba amesema, hadi wiki hii kwamba watu wawili
wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo, idadi ambayo alisema inaweza
kuwa kubwa zaidi endapo upimaji utafanyika katika kila wilaya za mkoa
huo. Lakini pengine watu wengi hawautambui ugonjwa wa homa ya Dengue upo
vipi, na hii ni kwa sababu ingawa ugonjwa huo upo katika maeneo yenye
hali ya hewa ya kitropiki au joto jingi lakini kwa nchi za Afrika
Mashariki ugonjwa huo haushuhudiwi sana.
Ugonjwa huo ni moja ya maradhi yanayosababishwa na virusi aina ya
Dengue vinavyoenezwa na mbu. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 50
huugua ugonjwa huu kila mwaka duniani huku watu wengi katika nchi 112
duniani wakiwa kwenye hatari ya kupata maambukizo. Kwa mujibu wa Shirika
la Afya Duniani WHO ugonjwa huu unaenezwa zaidi na mbu kuliko magonjwa
mengine ya virusi. Homa ya dengue pia hujulikana kama breakbone fever,
na maradhi hayo yamepewa jina hilo kwa sababu wahanga wa ugonjwa huu
mara nyingi hujikunja kutokana na maumivu makali ya viungo na misuli.
Homa ya dengue huenezwa na mbu wa jamii ya Aedes hasa aina ya Aedes
Aegypti. Aina hii ya mbu hupatikana kwa wingi katika maeneo yote ya
kitropiki na kwa karne kadhaa ugonjwa huu umekuwa ukishuhudiwa katika
nchi 12 za kusini mashariki mwa Asia na kusababisha vifo vya watu wengi
kila mwaka. Nchi nyingine ambazo homa ya dengue imeripotiwa ni katika
baadhi ya nchi za Afrika, Mexico, nchi za Amerika ya Latini kama Chile,
Paraguay na Argentina na pia kwenye visiwa vya Caribbean.
Kuna aina 5 ya virusi vya dengue vinavyosabisha maradhi hayo.
Maambukizi ya homa ya dengue hutokea baada ya mwanadamu kung'atwa na mbu
wa Aedes aliye na virusi vya dengue. Mbu huambukiza virusi hivyo pale
anapomg'ata mtu kwa kuingiza vijidudu hivyo kwenye damu, na kwa ajili
hiyo ugonjwa huu hauwezi kuenezwa moja kwa moja toka kwa mtu hadi kwa
mtu mwingine. Kwa kuwa kuna aina kadhaa za virusi vinavyosababisha homa
ya dengue, pale mtu anapoambukizwa virusi vya aina moja ya ugonjwa huo,
mwili wake hujenga kinga ya maisha kwa aina hiyo ya virusi, lakini
anaweza kuambukizwa homa ya dengui kutokana na virusi vya aina nyingine.
Miongoni mwa sababu zinazopelekea maambukizo ya maradhi hayo, ni
wahamiaji kuleta virusi hivyo vinavyosababisha homa hiyo na kusambazwa
ugonjwa huo na mbu. Pia watu wanaoishi katika makazi duni wapo kwenye
hatari ya kuathiriwa zaidi na homa ya dengue kwa sababu ya kuishi katika
mazingira yenye takataka nyingi na madimbwi ya maji machafu ambako mbu
huzaliana.
Dalili za homa ya dengue
Baada ya mtu kuambukizwa ugonjwa huu dalili hujitokeza baada ya siku 4
hadi 6 na huweza kudumu hadi siku 10. Mgonjwa huhisi homa kali
inayoweza kufikia nyuzi joto 41, kutetemeka na hupata maumivu makali ya
mgongo na viungo. Homa hudumu kwa siku 2-7 na homa inayodumu zaidi ya
siku 10 huenda ikawa haisababishwi na dengue. Dalili nyingine
zinazoambatana na homa hiyo ni maumivu ya kichwa, maumivu ndani au nyuma
ya macho, maumivu ya viungo, kichefuchefu na kutapika, vipele, uchovu,
kukosa hamu ya kula, maumivu ya koo, kuvuja damu isiyo nyingi katika pua
na fizi na kuvimba mitoki. Baadhi ya wakati dalili za homa ya dengue si
kali sana na zinaweza kukosewa na kuonekana kama mafua au maambukizo ya
virusi vingine. Baadhi ya wagonjwa wanaopatwa na homa hii huweza kupata
madhara zaidi kama vile homa inayoandamana na kuvuja sana damu, tatizo
linalotokea kwa nadra ambapo mgonjwa huwa na dalili zifuatazo, homa
kali sana, kuharibika mishipa ya damu, kutokwa damu puani na kwenye
fizi, ini kuwa kubwa na kushindwa kufanya kazi mfumo wa kupumua. Dalili
hizi zinaweza kuendelea na kusababisha damu kutoka kwa kiasi kikubwa,
kupata shock na kifo. Hali hiyo huitwa kitaalamu DSS yaani Dengue Shock
Syndrome. Watu wenye mfumo wa kinga ya mwili ulio dhaifu pamoja na wale
waliopatwa na maambukizo ya ugonjwa huu kwa mara ya pili au wale
wanaougua mara kwa mara na Homa ya Dengue wako katika hatari kubwa ya
kupatwa na shock ya aina hiyo.
Uchunguzi na matibabu
Baada ya dalili kujitokeza chunguzi hufanyika kwa lengo la kubaini
virusi vya dengue kwenye mwili. Vipimo kwa kawaida hufanywa kwenye
maabara kwa kutegemea dalili za mgonjwa na uchunguzi wa mwili na hasa
katika maeneo ambayo ugonjwa huo hushuhudiwa sana. Homa ya dengue
huthibitishwa kwa kipimo cha PCR kinachotumika kutambua virusi vya
ugonjwa huo. Kipimo hicho kinaweza kuonekana negativu mwanzoni mwa
maambukizo ya maradhi hayo. Hata hivyo vipimo vingine hutumika ili kujua
iwapo mgonjwa ana maradhi mengine au la.
Hakuna dawa ya kutibu homa ya dengue na mara nyingi ugonjwa huu
hukoma wenyewe bila matibabu yoyote. Mgonjwa anashauriwa kunywa maji ya
kutosha, kupumzika na kutumia dawa za kutuliza maumivu na kushusha homa
kama paracetamol. Pia mgonjwa wa homa ya dengue anapaswa kujiepusha
kunywa dawa kama vile asprin ambazo huzidisha kuvuja damu. Wagonjwa
wanaopata tatizo la kuvuja damu wanahitaji uangalizi wa karibu
hospitalini. Iwapo utaugua ugonjwa huo na kujihisi vibaya baada ya masaa
24 tangu homa kushuka, unapaswa kwenda haraka hospitali ili uchunguzwe
iwapo ugonjwa huo umesababisha madhara mwilini.
Hakuna kinga ya homa ya dengue na njia pekee ya kujikinga na ugonjwa
huo ni kuzuia kuenea virusi vya maradhi hayo kwa kupambana na mbu. Watu
wanashauriwa kujilinda wasipatwe na maambukizo ya ugonjwa huo kwa
kujizuia wasing'atwe na mbu wanaoeneza ugonjwa huo kutoka mtu mmoja hadi
mwingine. Pia kuweka mazingira katika hali ya usafi na kutoishi kwenye
mazingira yanayosaidia mbu kuzaliana kama madimbwi ya maji, vichaka,
maeneo ya mabondeni na yenye majani marefu na malundo ya takataka.
Zifuatazo ni njia tunazoweza kuchukua ili kuzuia mbu, ambao kama
tulivyosema ndio wanaosambaza na kueneza virusi vya homa ya dengue.
Kwanza kabisa ni kujizuia kung'atwa na mbu kwa njia mbalimbali kama vile
kuvaa nguo za kuzuia mbu wasitung'ate kama vile mashati ya mikono
mirefu na suruali pamoja na nguo ndefu zinazofunika mwili na kuzuia
kung'atwa na mbu. Pia kuzuia mbu wasiingie katika nyumba zetu kwa kuweka
nyavu kwenye madirisha, na kuwa na tabia ya kufunga madirisha ya nyumba
mapema kabla ya kuingia giza. Kutumia vyandarua katika vitanda wakati
wa kulala kila inapowezekana. Ni vizuri zaidi kutumia vyandarua
vilivyotiwa dawa ya kuua mbu. Tunaweza pia kujipaka dawa za kufukuza mbu
au kutumia na kufukiza dawa za kufukuza mbu majumbani ambazo hupatikana
kwa wingi katika maduka mbalimbali. Dawa za kujipaka za kufukuza mbu ni
salama kwa watoto na mama wajawazito, lakini tunashauriwa kuwa
waangalifu na kuhakikisha kwamba dawa hiyo haigusi macho na midomo. Njia
nyingine ya kuwaepuka mbu ni kuwa na tabia ya kusafisha mazingira
yanayotuzunguka, kwa kukata majani marefu, kufukia vidimbwi vya maji
vinavyowavutia mbu kuzaana kwa wingi, kutia dawa za kuulia mbu kwenye
mashimo ya vyoo, maji yaliyosimama na kadhalika.
Naam wapenzi wasikilizaji, tukumbuke kuwa, kinga daima ni bora kuliko
tiba, hivyo tujitahidi kutong'atwa na mbu ili tusipatwe na homa hatari
ya Dengue.







No comments:
Post a Comment