Mizozo na mivutano kati ya
makundi ya upinzani yanayobeba silaha nchini Syria inazidi kuongezeka
siku baada ya siku. Kushtadi migogoro hiyo kunakwenda sambamba na
mafanikio makubwa ya jeshi la Syria katika kupambana na magaidi nchini
humo. Kuhusiana na hilo, As'ad Mustafa Waziri wa Ulinzi wa serikali eti
ya muda ya wapinzani amelazimika kujiuzulu baada ya kuzuka hitilafu
kubwa kati yake na Ahmad Jurba mkuu wa muungano unaojiita Syrian
National Coalition (SNC).
Kabla ya hapo Sami Al-Oraidi kiongozi wa kundi
la Jabhat an-Nusra alisema kuwa, Ahmad Jurba mkuu wa Muungano wa
Kitaifa wa Syria SNC ameiba dola milioni 75 zilizotolewa kama msaada kwa
makundi ya upinzani nchini Syria.
Vile vile sambamba na
kushadidi hitilafu na mivutano baina ya makundi ya kigaidi yaliyoko
Syria, Riyadh As'ad mwasisi wa kundi la kigaidi la Jeshi la Ukombozi wa
Syria naye ametoa wito wa kuvunjwa kundi hilo akisema kwamba, viongozi
wake hawana wanachofikiria ghairi ya pesa na madaraka. Wachambuzi wa
mambo wanaamini kwamba, licha ya kuweko misaada ya madola ya Magharibi
na Saudi Arabia kwa magaidi wa Syria, lakini mwenendo wa kushindwa
magaidi na jeshi la Syria unaendelea kushuhudiwa na kuonekana zaidi
kadiri siku zinavyosonga mbele, jambo ambalo linatajwa na wajuzi wa
mambo kwamba, limewafanya viongozi wa makundi hayo ya kigaidi
wachanganyikiwe na kuanza kuparurana wao kwa wao. Aidha katika mlolongo
wa kushadidi hitilafu kati ya wapinzani wa Syria, hivi karibuni kundi
la kigaidi linalojiita Serikali ya Kiislamu ya Iraq na Sham (DAESH)
lilimuua kwa kumkata kichwa mmoja wa viongozi wa kundi jingine
lilalojulikana kwa jina la Ukombozi wa Sham. Hii ni katika hali ambayo,
chombo kimoja cha habari cha Uingereza kimefichua jinai za kutisha
zinazofanywa na makundi ya kigaidi ya Syria na kubainisha kwamba,
vitendo vya makundi hayo vinashahibiana na makundi ya kimafia. Duru za
Syria kwa upande wake zimeashiria juu ya kutokuweko malengo mamoja kati
ya makundi ya kigaidi nchini humo na kufichua pia mizozo iliyopo hivi
sasa kati ya nchi zinazoyaunga mkono makundi hayo ya kigaidi na
kusisitiza kwamba, kile ambacho leo kinatokea nchini Syria ni ugaidi wa
kimataifa wa baadhi ya nchi za Kimagharibi na Kiarabu.
Ukweli wa mambo ni kuwa,
kadiri siku zinavyosonga mbele, ndivyo yanavyothibitisha wazi maneno ya
viongozi wa Syria kwamba, nchi hiyo iko katika vita na makundi ya
kigaidi ambayo yanapata himaya na uungaji mkono kutoka kwa madola ya
Magharibi yanayodai kuwa vinara wa kutetea haki za binadamu ulimwenguni.







No comments:
Post a Comment