Jeshi la Thailand jana Jumanne
lilitangaza kushika majukumu ya kulinda nchi lakini limesisitiza kuwa
hatua hiyo si mapinduzi ya kijeshi. Habari zinasema jeshi limetangaza
sheria kali ikiwa ni pamoja na kutishia kuwatia mbaroni wanaochochea
fujo pamoja na kuzuia vyombo vya habari kutangaza baadhi ya mambo. Mkuu
wa jeshi la Thailand, Prayuth Chan-Ocha amesema kwa sasa masuala yote ya
usalama yako mikononi mwa jeshi na amezitaka pande za kisiasa
zinazohasimiana kufanya mazungumzo mara moja na kutatua hali ya mambo.
Pia kanali 10 za televisheni zimefungwa kwa muda. Waziri Mkuu wa
serikali ya mpito ya nchi hiyo, amesema jeshi halikumshauri kabla ya
kuchukua udhibiti wa nchi.
Maandamano makubwa yameshuhudiwa nchini
Thailand kwa miezi 6 iliyopita ambapo wafuasi wa upinzani na wale wa
serikali wamekuwa wakikabiliana katika mji mkuu, Bangkok. Maandamano
hayo yaliyogubikwa na ghasia yamesababisha zaidi ya watu 25 kupoteza
maisha. Wapinzani wamekuwa wakishinikiza Waziri Mkuu, Yingluck
Shinawatra, ajiuzulu huku wafuasi wa mwanasiasa huyo wakisisitiza
kuendelea utawala wake. Hata hivyo, mwanzoni mwa mwezi huu, mahakama ya
kilele ilimuuzulu Bi. Shinawatra baada ya kumpata na hatia ya kutumia
vibaya mamlaka yake.







No comments:
Post a Comment