Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Wednesday, May 14, 2014

Indhari kuhusu sheria ya Wazayuni ya kuugawa msikiti wa al-Aqsa

Waziri wa Waqfu na Masuala ya Kidini wa serikali halali iliyochaguliwa na wananchi huko Palestina ametahadharisha juu ya njama mpya za utawala wa Kizayuni wa Israel za kutaka kuugawa msikiti wa al-Aqsa. Ismail Ridhwan amelaani hatua ya walowezi wa Kizayuni ya kuuvamia msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kusema kuwa, Wazayuni wanalenga kuvuruga hali ya mambo katika mji wa Quds ili wadhibiti kikamilifu Masjidul Aqsa. Hapo jana Jumanne, Walowezi wa Kizayuni wakisaidiwa na jeshi la utawala ghasibu wa Israel walivamia msikiti wa al-Aqsa kwa upande wa magharibi kupitia 'Babul Maghariba' na kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu kwenye msikiti huo. Msikiti huo mtakatifu wa Waislamu umekuwa chini ya hujuma ya mara kwa mara ya Wazayuni jambo linaloendelea kuwakera Waislamu kote duniani.

Huku Wapalestina wakikaribia kukumbuka miaka 66 tangu utawala wa Kizayuni uzikalie kwa mabavu ardhi zao, utawala huo bandia pamoja na walowezi wa Kizayuni wameweka mikakati ya kuwazuia kufika katika msikiti wa al-Aqsa kwa ajili ya maadhimisho hayo.
Pia katika kukaribia safari ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis huko Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu, Utawala wa Kizayuni umezuia kuwekwa mabango ya kumkaribisha kiongozi huyo wa kidini huko. Hatua hiyo imeikasirisha mno jamii ya Wakristo huko Quds. Dimitry Dalyani, Katibu Mkuu wa makundi ya Kikristo katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu amesema Waislamu na Wakristo wa mjini Quds wanapaswa kushirikiana bega kwa bega kupinga njama za Wazayuni za kutaka kuuyahudisha msikiti wa al-Aqsa na mji wa Quds kwa ujumla.
Papa Francis I anatarajiwa pia kutembelea eneo la Beit al-Laham au kwa jina jingine Bethlehem lililoko ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na tayari maandalizi yamekamilika ili kumpokea kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani. Duru zinaarifu kuwa, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas atakutana na Papa wakati wa ziara yake hiyo ambapo watajadili njama zinazofanywa na Israel za kuharibu turathi za kidini na kubadilisha muundo wa mji wa Quds. Hii ni katika hali ambayo, Bunge la utawala haramu wa Israel limeandaa muswada wa sheria unaolenga kuugawa msikiti wa al-Aqsa. Tayari muswada huo umekabidhiwa baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni  kwa ajili ya kuidhinishwa.  Sheria hiyo ikipitishwa, itatoa idhini kwa Mayahudi kuingia katika msikiti huo na kuendeshea humo shughuli zao.
Utawala ghasibu wa Israel baada ya kughusubu mji wa Quds kwenye vita vya siku 6 vya mwaka 1967 ulianza kuharibu matukufu ya kidini ya Waislamu na Wakristo wa Palestina katika mji huo ikiwa ni pamoja na Masjid al-Aqsa na kanisa mashuhuri zaidi mjini hapo.

No comments: