Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Monday, September 17, 2012

Miradi ya nyuklia ya Israel, ajenda ya kikao cha IAEA

Kujadiliwa miradi ya nyuklia ya utawala wa kizayuni wa Israel ni miongoni mwa ajenda za kikao cha 56 cha kila mwaka cha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kilichoanza leo huko mjini Vienna. Licha ya hatua za Marekani, utawala wenyewe wa kizayuni na baadhi ya nchi za Magharibi ya kutaka kuunyamazisha Wakala wa IAEA usilifuatilie faili la nyuklia la Israel ripoti zinaeleza kuwa, kutokana na sisitizo la nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM pamoja na nchi za Kiarabu faili la nyuklia la utawala haramu wa Israel litawekwa tena kwenye ajenda za kujadiliwa katika kikao cha IAEA.
Kadhia ya nyuklia ya utawala wa kizayuni imepangwa kujadiliwa katika hali ambayo kwa mujibu wa azimio lililopitishwa katika mkutano wa mwaka 2009 wa IAEA utawala haramu wa Israel ulitakiwa ujiunge na mkataba wa kuzuia uundaji na uenezaji silaha za nyuklia NPT na kuruhusu vituo vyake vya nyuklia viwe chini ya ukaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Inafaa kuashiria hapa kuwa kwa muda mrefu sasa taathira hasi za kuendelea shughuli za nyuklia na kijeshi za utawala wa kizayuni katika nyanja mbalimbali zimezusha wasiwasi mkubwa kieneo na kimataifa. Kutokana na Israel kuzalisha na kurundika chungu ya silaha za atomiki katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu pamoja na silaha za kemikali imeligeuza eneo la Mashariki ya Kati kuwa ghala kubwa la silaha za mauaji ya halaiki. Hivi sasa utawala wa kizayuni unakadiriwa kuwa na idadi ya vichwa vipatavyo 300 vya atomiki na ndio utawala pekee katika eneo hili ambao umekataa kusaini mkataba wa NPT. Si hayo tu lakini utawala huo haramu umekataa kata kata kuruhusu vituo vyake vya nyuklia vikaguliwe na wakaguzi wa IAEA. Ukiukaji wa mara kwa mara wa sheria za kimataifa na hasa kanuni zinazohusiana na shughuli za nyuklia unaofanywa na utawala wa kizayuni na waungaji mkono wake unahatarisha mno amani na usalama wa eneo na ulimwengu mzima. Kwa sababu hiyo nchi nyingi za eneo na ulimwengu kwa jumla zinataka jumuiya za kimataifa na hasa taasisi husika kama Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki uchukue hatua dhidi ya utawala wa kizayuni. Kwa mtazamo wa weledi wa masuala ya kisiasa, badala ya maafisa wa IAEA kukubali ushawishi wa Marekani na nchi za Magharibi na kufuata siasa zao za kutaka kuzinyima nchi za eneo la Mashariki ya Kati haki yao ya kunufaika na nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani wanapaswa kukusanya nguvu na suhula za wakala huo ili kuhakikisha jamii ya kimataifa inachukua hatua kali na za maana za kukabiliana na miradi ya nyuklia na ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni.

No comments: