Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, June 5, 2012

Kuendelea jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya mateka wa Kipalestina na ahadi tupu za Umoja wa Mataifa

Kuendelea jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya mateka wa Kipalestina wanaozuiliwa katika jela za kuogofya za utawala huo kunaendelea kukabiliwa na radiamali tofauti kutoka ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo na vilevile katika ngazi za kimataifa. Katika upande wa ndani, Issa Qaraqe' Waziri wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina anayeshughulikia Masuala ya Mateka na Wakimbizi amesema mateka wa Kipalestina wametishia kurejea mgomo wao wa chakula kutokana na vitendo vya mabavu wanavyofanyiwa na utawala huo wa Kizayuni. Amesema utawala huo umekiuka wazi mkataba ulioutia saini hivi karibuni na mateka hao, kwa kuanzisha tena operesheni za kuwatia nguvuni mateka bila kuwafikisha mahakamani.
Mwezi Mei uliopita utawala haramu wa Israel ulitiliana saini na viongozi wa maelfu ya mateka wa Palestina ambao tokea mwezi Februari walianza kususia chakula, na kuahidi kwamba ungeshughulikia malalamiko yao baada ya wao kuamua kusitisha mgomo wa chakula. Licha ya makubaliano hayo lakini utawala huo ungali unawatia nguvuni mateka na kuwakandamiza. Suala hilo limeamsha radiamali ya kimataifa dhidi ya utawala huo ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutokana na ombi la Wapalestina, limekubali kufanya kikao cha dharura kwa lengo la kuchunguza malalamiko ya wafungwa wa Kipalestina na uwezekano wa kupelekwa faili la jinai za utawala huo katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Hata hivyo tarehe ya kufanyika kikao hicho bado haijatangazwa.

Kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na hasa mateka wao kumechukua mkondo mpya na hatari katika siku za hivi karibuni. Zaidi ya mateka 5000 wa Kipalestina wanaendelea kuteseka katika jela za utawala huo na hii ni katika hali ambayo mateka wapya wamekuwa wakikamatwa na kurundikwa kwenye jela hizo za kuogofya.
Wafungwa wa Kipalestina zaidi ya 200 wamepoteza maisha yao na mamia ya wengine kukumbwa na magonjwa sugu yasiyotibika katika miaka ya hivi karibuni kutokana na mateso makali wanayopata katika jela hizo. Kuendelea kwa jinai na kukanyagwa kwa haki za kimsingi za Wapalestina ni jambo linaloendelea kuhatarisha maisha yao kila siku.
Katika hali hiyo kimya cha jamii ya kimataifa kimeupelekea utawa huo wa Kizayuni kumea pembe na kuendelea kutenda jinai dhidi ya taifa la Palestina bila kujali lolote. Inasikitisha kuona kwamba kila mara mashinikizo ya kimataifa yanapoongezeka dhidi ya jinai za utawala huo dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina, taasisi za kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa hutoa ahadi tupu za kufuatilia jambo hilo na kisha kutofanya lolote muhimu baada ya kupungua mashinikizo hayo. Fikra za waliowengi duniani zinataka kutatuliwa haraka na tena kwa uadilifu suala la Palestina na kwa hivyo tasisi na mashirika husika ya kimataifa yanapasa kulishughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo.

No comments: