Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, May 1, 2012

EAC watakiwa kupambana na fedha haramu

NCHI wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinatakiwa kuunganisha nguvu zao kwa pamoja, ili kupambana na fedha haramu na ongezeko la ufadhili wa vitendo vya kigaidi katika kanda hiyo.

Waziri wa Usalama wa Burundi, Gabriel Nizigama alisema hayo jana wakati wa kufungua warsha ya siku nne ya wataalamu fedha haramu na ufadhili wa ugaidi, mjini Bujumbura, Burundi.

‘’Nchi za EAC zinaweza kufanikiwa katika kuzuia na kupambana na fedha haramu na ufadhili wa ugaidi kupitia juhudi za pamoja,’’ alisema.
Alisema nchi hizo zinahitaji hatua maalumu ya kutambua na kuzuia shughuli za kihalifu kupitia uhifadhi wa kumbukumbu, utambuzi wa wateja na utoaji taarifa haraka kuhusu shughuli au watu wanaotiliwa mashaka.

Warsha hiyo inayohudhuriwa na wataalamu wa kupambana na fedha haramu, Kitengo cha Usalama wa Fedha, mamlaka za mapato, wanasheria, polisi na maofisa usalama imeandaliwa na EAC kwa kushirikiana na Serikali ya Australia.

Warsha hiyo ni matokeo ya uamuzi wa mkutano wa nne wa Baraza la Kisekta la Usalama ambalo lilitambua kwamba fedha haramu ni tishio kwa mtangamano wa EAC.

Naibu Katibu Mkuu wa EAC, anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Beatrice Kiraso alisema kadiri mtangamano wa EAC unavyozidi kuimarika, ni dhahiri kuwepo kwa vitendo vya uhalifu hakukwepeki.

‘’Tuna wajibu wa kulinda miundombinu yetu ya fedha na utulivu wa uchumi wetu kama manufaa ya mtangamano wetu yanatakiwa yaonekane,’’ alisisitiza na
kuongeza kwamba uhalifu kama usafirishaji wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya kigaidi lazima vipigwe vita vikali.

“Vinginevyo uhalifu huo utaharibu maendeleo ya kiuchumi ndani ya ukanda, kuwatisha wawekezaji na kuharibu usalama na utulivu uliopo ndani ya nchi za EAC,” alisema Kiraso katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mtaalamu wa EAC wa Masuala ya Amani na Usalama, Leonard Onyonyi.

Mwakilishi wa Serikali ya Australia, Mike Petty alisema ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa sababu utandawazi siyo tu kwamba unaleta teknolojia na jamii pamoja bali pia wahalifu na uhalifu hatari.

No comments: