Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Monday, April 2, 2012

‘Umbumbumbu chanzo cha miaktaba mibovu Afrika’

MRATIBU Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Alberic Kacou amesema ubovu wa mikataba mingi ya rasilimali Afrika unatokana na Serikali za nchi hizo kutokuwa na uelewa wa kutosha wakati wa mazungumzo pamoja na kutokuwa wazi kwa wananchi wake.

Kacou alisema ili kuondoa matatizo hayo, serikali za nchi hizo zinatakiwa kuwa wazi wakati zinaingia katika mikataba hiyo kwa kupitia Bunge na vyombo vya habari.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika majadiliano maalumu kati yake na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya  IPP Media, Reginald Mengi, Kacou alisema endapo Serikali hizo zitaweka wazi mikataba hiyo, wananchi wataondoa chuki dhidi ya Serikali zao.

“Nchi nyingi za Afrika hasa zinazoendelea zinaingia katika mikataba mibovu ya rasilimali zake kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha wakati wa mazungumzo,” alisema Kacou na kuongeza;
“Nchi hizi za Afrika zina rasilimali nyingi sana lakini zinashindwa kuzitumia kutokana na kuingia katika mikataba hii mibovu.”

Aidha, mratibu huyo wa UN alisema wawekezaji mbalimbali pia wanashindwa kuja kuwekeza katika nchi za Afrika kutokana na kuwa na matatizo ya umeme pamoja na miundombinu mibovu.

Mwakilishi huyo wa UN ambaye yupo nchini Tangu mwaka 2009, pia aliisifu Tanzania kwa kuwa na amani na kuwa na utajiri wa rasilimali mbalimbali. Kacou alisema uchaguzi mkuu wa rais uliopita ulifanyika kwa amani na hatua hiyo ni mfano mzuri wa kuigwa katika nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Matokeo ya urais Senegal
Akizungumzia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Rais yaliyotangazwa juzi nchini Senegal ambapo mgombea wa upinzani, Macky Sall aliibuka mshindi, Kacou aliupongeza uchaguzi huo pamoja na kumpongeza aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Abdoulaye Wade kwa kuyakubali matokeo.

“Nina furaha kubwa baada ya kuyapata matokeo, kauli ya wananchi lazima iheshimike, na matokeo yaheshimike, na pia nampongeza Rais Wade kwa kuyakubali matokeo hayo” alisema Kacou.

No comments: