Katika hali ambayo wananchi wa Bahrain wanakandamizwa vikali huku vitendo vya kikatili na ukandamizaji vya utawala wa ukoo wa Aal Khalifa dhidi ya wananchi hao vikiendelea kila siku kuchukua sura mpya, Salman bin Hamad Aal Khalifa, mrithi wa kiti cha ufalme amefanya safari kuelekea nchini Marekani. Huko mjini Washington Salman bin Hamad ameonana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton ambaye mbali na kutangaza uungaji mkono kwa utawala wa Aal Khalifa amesema Bahrain ni muitifaki wa Marekani mwenye thamani. Kuwepo manowari ya Marekani huko Bahrain kumeifanya nchi hiyo kuwa mmoja wa waitifaki muhimu wa Washington katika eneo hili la Ghuba ya Uajemi.
Tangu tarehe 14 Februari mwaka uliopita wakati malalamiko ya wananchi dhidi ya utawala wa kidhalimu na wa kibaguzi wa Bahrain yalipopamba moto na kudhihirishwa waziwazi, Marekani imekuwa miongoni mwa nchi zinazotoa uungaji mkono mkubwa kwa utawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Hivi sasa mamia ya anuwai za silaha za Marekani ziko mikononi mwa vikosi vya usalama vya utawala wa Manama zikitumiwa dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Bahrain. Wataalamu wengi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa mauaji ya raia wa Bahrain yaliyofanywa hadi sasa tangu lilipoanza vuguvugu la mapinduzi yamepata baraka za Marekani. Washington inachelea kupoteza kituo chake cha kijeshi endapo mapambano ya wananchi wa Bahrain yatapata ushindi. Kwa sababu hiyo inatumia kila mbinu ili kuulinda utawala wa Aal Khalifa na kuhakikisha unaendelea kubaki madarakani. Wakati Marekani inajinasibu kila mara kuwa mtetezi wa haki za binadamu, lakini kwa sababu ya kulinda maslahi yake imeamua kunyamazia kimya ukandamizaji uliofanywa na unaoendelea kufanywa huko Bahrain na utawala wa Aal Khalifa. Na hii ni katika hali ambayo msimamo wa Washington kuhusiana na mgogoro wa Syria ni tofauti kabisa na ule wa Bahrain. Kwa hakika kadhia hii moja tu inatosha kubainisha upeo wa uzandiki na undumakuwili katika misimamo ya Marekani kuhusiana na matukio ya eneo hili. Katika kile kinachoonekana kama janja ya kuzihadaa fikra za waliowengi duniani na kwa kuonesha hisia za kiutu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amemtaka mrithi wa Ufalme wa Bahrain kuchukua hatua za kivitendo za kutekeleza mageuzi ya msingi nchini humo. Kwa kuzingatia kwamba utendaji wa utawala wa Aal Khalifa daima umekuwa ni wa kufuata na kukidhi matakwa ya Marekani hivyo hakuna chembe yoyote ya shaka kuwa hivi sasa pia utaamiliana na wananchi wa Bahrain wanaopinga utawala huo kulingana na maagizo na maelekezo aliyopewa Salman bin Hamad Aal Khalifa huko Washington
Subscribe to:
Post Comments (Atom)







No comments:
Post a Comment