Leo ni Jumatatu tarehe 22 Shaabani mwaka 1434 Hijiria, inayosadifiana na Julai Mosi mwaka 2013 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, nchi ndogo ya Burundi
ilijitangazia uhuru wake. Ardhi ya Burundi pamoja na Rwanda ilikuwa
sehemu ya makoloni ya Mjerumani huko Afrika Mashariki kuanzia mwaka 1899
hadi 1917. Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kushindwa
Ujerumani katika vita hivyo, Umoja wa Mataifa uliikabidhi Ubelgiji ardhi
ya Burundi na mwaka 1946, ukatambuliwa rasmi utawala wa Ubelgiji kwa
nchi hiyo. Mwaka 1962 Burundi ilipata uhuru ikiwa na mfumo wa utawala wa
Kifalme. Hata hivyo miaka minne baadaye wapigania jamhuri walimuondoa
madarakani mfalme na kuanzisha mfumo wa serikali ya jamhuri.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, sehemu mbili za
Somalia ya Uingereza na ya Italia ziliungana na kuunda nchi moja ya
Somalia yenye kujitawala. Karne kadhaa nyuma, Somalia iliwahi kujitawala
kwa kipindi kifupi. Mwaka 1884 Uingereza iliiweka katika himaya yake
sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Miaka mitano baadaye Italia nayo ikakoloni
baadhi ya sehemu za Somalia. Harakati za mapambano za Muhammad Abdullah
Hassan dhidi ya Waingereza kuanzia mwaka 1901 hadi 1920 hazikusaidia
kitu. Mwaka 1950 Umoja wa Mataifa uliitaka Italia iandae mazingira ya
kujitawala na kuwa huru Somalia.
Na miaka 51 iliyopita siku kama ya leo, nchi nyingine ya
Kiafrika ya Rwanda ilipata uhuru. Rwanda ina historia inayofanana na
jirani yake wa kusini yaani Burundi ambapo kabla ya nchi hizo
kujitangazia uhuru zilikuwa zikikoloniwa na Ubelgiji. Mwaka 1973,
Meja-Generali Juvenal Habyarimana aliingia madarakani baada ya kufanya
mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu. Baada ya mapambano mtawalia ya
wapigania uhuru wa Rwanda, hatimaye mnamo mwaka 1962, nchi hiyo ilipata
uhuru na kabila kubwa kabisa nchini humo la Wahutu likashika hatamu za
uongozi wa nchi. Hata hivyo mwaka 1994 kulitokea mauaji ya kimbari
ambapo zaidi ya watu laki 8 waliuawa wengi wao wakiwa ni wa kabila la
Kitutsi.
No comments:
Post a Comment