Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, April 14, 2013

Kisanga cha kukamatwa kwa Tido Mhando nchini Kenya

Tido, akiwa bado anaishi nchini Kenya, na  baada ya kuwa mwandishi wa habari wa kwanza kutangaza kuuawa kinyama kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Kenya, Dr. Robert Ouko,  aliamua kuchukua nafasi ya mwaliko aliopatiwa na BBC kwenda London kwa ziara ya mafunzo ya miezi mitatu. Akiwa kwenye maandalizi ya safari hiyo, alienda kwanza Dar es Salaam kuaga wazazi.  Huku nyuma, maafisa wa Usalama wa Serikali ya Kenya walienda kumtafuta ofisini kwake mjini Nairobi kwa nia ya kumkamata.  Sasa endelea…
Wafanyikazi wa ofisi za jirani na ile ya VOA niliyokuwa nikifanyia kazi pale Chester House, Nairobi, na wao hawakujua nilipokuwa, kwani niliondoka bila ya kuwaaga.
Halikadhalika, wale wafanyikazi wengine wote niliokuwa nikifanya kazi nao ofisi moja walikuwa kwenye likizo zao, hivyo ofisi za VOA zilikuwa zimefungwa. Kwahiyo, hao jirani zangu wakawa wanatapatapa kutafuta njia ya “kunitonya” kwamba nisiende ofisini maana natafutwa.

Wakiwa kwenye lindi la mtihani huo, mmoja wao  akamkumbuka rafiki yangu mkubwa ambaye alikuwa na tabia ya kunitemebelea pale ofisini mara kwa mara. Yeye na wenzie wakaona kwamba huyo lazima angejua pale nilipo, hivyo wakamtafuta na kumfahamisha hali ya mambo.
Ilikuwa majira ya saa tano mchana hivi wakati nilipowasili nyumbani kwa wazee wangu Chang’ombe. Wakati bado tunajuliana hali, ghafla nikaambiwa kuna simu inayonitafuta. Nikashangaa huku najiuliza: ni nani huyo ambaye mara hii keshafahamu kwamba nimewasili Dar?Nikaambiwa alikuwa ni rafiki yangu wa Nairobi, Livingstone Amaumo.  Nikashangaa zaidi.
Livingstone alikuwa rafiki yangu mkubwa sana kwa kipindi chote nilichokuwepo nchini Kenya. Yeye alikuwa meneja kwenye kampuni kubwa ya kimataifa ya kurikodi na kuuza nyimbo, CBS.
Wakati ule ni nyimbo za sahani za santuri. Alikuwa mtu mpole sana, mnyenyekevu mno, mkarimu kupita kiasi. Muungwana kweli kweli. Akipenda sana muziki wa Kitanzania.
Kwakuwa nilikuwa nafahamiana na wanamuziki maarufu karibu wote Watanzania wakati huo, wakina: Muhidini Gurumo, Hassan Bitchuka, Ndala Kasheba, Kiki, Maneti, Juma Kilaza, Nguza Viking,Cosmas Tobias Chidumule, Marijani Shabani, Chinyama Chiaza aliyekuwa kiongozi wa Orchestra Maquisdu Zaire nyakati hizo, Patrick Balisidya wa Afro 70 Band, na wengine wengi, nilimunganisha nao.
Wakati mmoja tuliwachukua baadhi ya wanamuziki wa kikundi cha Mlimani Park Orchestra, kikiwa bado kipya siku hizo, wakaja Nairobi kurikodi nyimbo kadhaa, ndipo wimbo wao wa “Nawashukuru Wazazi” ukavuma sana sana nchini Kenya.
Kwakweli Livingstone alikuwa zaidi ya rafiki. Alikuwa ni kama ndugu yangu wa Kikenya. Aliwafahamu ndugu zangu wote na jamaa zangu kadhaa. Alipenda sana kuja kutembea Tanzania.Aidha, hakuupenda tu muziki wa Kitanzania bali pia aliipenda sana Tanzania kwa ujumla wake hata wakati  mkewe alipojifungua mtoto wao wanne wa kiume na wamwisho, wakamuita Nyerere.
Nikachukua simu ya Livingstone na kauli yake ya kwanza kabisa ikawa:“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba upo huko.” Nikamwuliza, “Kwani kuna nini?” Ndipo alipoponifahamisha kisanga kile cha mimi kutafutwa na jamaa wa usalama. Nikapigwa na ganzi.
Kwa muda mfupi uliofuata nikawa natafakari hili na lile. Nikajisemea kimoyomoyo: “Hawa jamaa wananitafutia nini? Wanataka tu kunitia matatani bila ya sababu yoyote ya maana? “Wanataka tu kuniharibia maisha yangu na ya watoto wangu waliokuwa wadogo bado!”
Watoto wetu tuliwaacha pekee yao Nairobi kwani tulikuwa tumepanga kurejea huku baada ya muda mfupi tu. Niliamua kujinyamazia, bila ya kumwambia na kumtia taharuki, Mwangaza, mke wangu.
Lakini wakati nikiendeleakuwaza na kuwazua, simu ya pale nyumbani ikalia kwa mara nyingine. Nikaambiwa tena ilikuwa simu yangu. Nikadhani labda ni Livingstone yule rafiki yangu, labda kasahau jambo. Lakini nilipoichukua ikawa ni simu kutoka ubalozi wa Marikani, Nairobi.

No comments: