Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, April 29, 2012

Nyama ya mamba yageuka lulu Bagamoyo

MWENDO wa kilomita tatu kutoka Bagamoyo mjini kuelekea mji wa Kaole, wenye  utajiri mkubwa wa vivutio vya asili vinavyoaminika kuwapo eneo hilo kwa zaidi ya miaka 500  iliyopita, unafika eneo maarufu kwa ufugaji wa mambalinalojulikana kama Kaole Mamba Ranch.

Hapa kuna Mamba wengi wa saizi mbalimbali wanaofugwa. Kinachovutia zaidi ni kwamba, eneo hilo pia kuna machinjio maalumu ya mamba kwa ajili ya kitoweo kwa mtu yeyote unayehitaji.

Shamba hili linalomilikiwa na wazawa, lilianzishwa mwaka 1992 kwa madhumuni ya kufuga na kuuza ngozi za viumbe hao hatari kwa maisha ya binadamu, ambao uchunguzi unaonyesha watu zaidi ya 500 huuawa kila mwaka duniani kutokana na kushambuliwa na mamba.

Hata hivyo, kupanuka kwa mahitaji ya binadamu na kubadilika kwa mifumo ya maisha, kulifungua milango ya uuzwaji nyama ya mamba baada ya kuongezeka kwa walaji wake.

Ingawa mamba ni hatari kwa maisha ya binadamu kutokana na kumfanya kama sehemu ya chakula chake, upande wa pili naye binadamu amemfanya kitoweo.


Jinsi mamba wanavyochinjwa
Katika shamba hili, kwa mlaji wa nyama hiyo anachofanya ni kutembelea kwenye mabanda wanayofugwa, kisha kuchagua unayehitaji na baada ya mapatano ya bei, unachinjiwa hapohapo na kuondoka na nyama yako.

Peter Mamba, Msimamizi wa shamba hilo anasema kazi ya kumchinja mamba ni rahisi kama kuchinja kuku ili mradi tu awe amefungwa mdomo, miguu na mkia sehemu ambazo ni hatari.

"Mamba hata kama ni mkubwa kiasi gani, anaweza kuchinjwa kirahisi lakini kwanza kwa kuhakikisha amefungwa mdomo na mkia kwani ndiyo maeneo hatari anayoweza kumjeruhi binadamu," anasema.

Katika shamba hilo, kuna sehemu maalumu imetengezwa kwa sementi na kwa muonekana sehemu hiyo inafafana na kibaraza kidogo, ambapo mamba baada ya kukamatwa toka kwenye banda hupelekwa hapo kuchinjwa na kuchunwa ngozi.

Anasema mamba hukamatwa kwa mitego maalumu na kuondolewa bandani kwa kufungwa sehemu hizo na kulazwa eneo la kuchinjwa, ambapo zoezi zima linaweza kuwa chini ya dakika 10.

Utafiti wa kitaalamu unaonyesha kuwa, nyama ya mamba ina ladha kama kuku na ina madini mengi ya joto ambayo binadamu huhitaji zaidi kwa ajili ya ustawi wa afya yake.

Nyama ya mamba ina proteni nyingi, kama vitamini B 12, haina mafuta (cholesterol) na ina ladha kama nyama ya Kuku. Inaelezwa kuwa, ni bora zaidi kula nyama ya mamba kuliko ng'ombe au nguruwe.

Walaji

Peter anasema walaji wakubwa wa mamba ni raia kutoka China na wazungu wachache, na ameshangazwa na utamaduni wa Waafrika kutopenda kujaribu kuonja vyakula vingine kama nyama ya mamba.

"Mimi binafsi nimewahi kula Mamba, ana nyama nzuri na tamu haswa. Mamba ana nyama nyeupe, haina damu kama alivyo kuku, hakuna tofauti kati ya nyama ya Mamba na Kuku,"anasema Peter.

Peter anasema watu wengi wanashangaa kusikia mamba analiwa na hii ni kwa sababu ya utamaduni wa kutopenda kujaribu mambo mapya miongoni mwa watu wengi.

"Hapa wanakuja watu wengi kutembelea kwa lengo la kuona ufugaji huu, lakini tukiwaeleza kwamba tunauza pia viumbe kwa ajili ya kitoweo, wengi hushangaa kwa kumuona mamba kama kiumbe aliyekosa sifa za kuliwa," anasema Peter.
Anasema kutokana na watu wengi kutopenda nyama ya mamba, kumefanya soko lao kuwa gumu kwani wanalazimika kuwategemea wateja wao wa siku zote ambao ni wachache na wakati mwingine huja mara moja baada ya zaidi ya mwaka.

"Tunauza mara moja moja sana nyama ya mamba, kiasi tunauza Nairobi Carnival na Uarabuni. Ukweli ni kwamba, soko limepungua kwa kiasi kikubwa hapa nchini."

Changamoto nyingine ya kukosekana kwa soko ni kutokana na nyama hiyo kuuzwa bei kubwa, ambapo kila moja huuzwa Sh150,000 jambo ambako kwa wengi ni ngumu.

Kuhusu utunzaji wa mamba kwenye shamba hilo, Msimamizi Msaidizi, Cosmas Joseph anasema wana mamba zaidi ya 200, wakubwa kwa wadogo, ambapo mkubwa zaidi ana miaka 54.

Joseph anasema mamba anaweza kuishi hata zaidi ya miaka 150, na wale wanaopatikana Afrika (Nile Crododile) ndiyo wanaelezwa kuishi miaka mingi kuliko aina nyingine ya mamba.

Kitaalamu, kuna aina 15 za mamba zinazotambulika ambapo sehemu kubwa ya aina hizo, zinapatikana zaidi katika nchi za kitropiki zikiwemo baadhi ya nchi Afrika, Asia na Marekani.

Mamba mkubwa kabisa anajulikana kitaalamu kama 'Crocodylus porosus' na hupenda kuishi kwenye maji ya chumvi akiwa na urefu unaofika mita saba (sawa na futi 23 au zaidi) Hawa wanapatikana sana India na Australia.

Mamba wengine wenye sifa ya ukubwa, ni wale wanaojulikana kama Nile crocodile wanaopatika sehemu kubwa barani Afrika ambao wanaweza kufika urefu wa futi 15 (sawa na mita 4.6).

Aina nyingine japo kuzitaja chache ni Cuban crocodile, Morelet crocodile, Tomistoma schlegelli na Guinea crocodile. Mamba wote wana tabia zinazofanana kutegemea na mazingira wanayoishi.

Akieleza tabia za mamba anasema, ni kiumbe asiyekuwa na urafiki siyo tu na viumbe wengine bali hata wao wenyewe kwa wenyewe. "Mamba akikosa chakula, anakamata mamba mdogo na kumla, ndiyo maana unaona hapa tumewatenganisha kutokana na umri na maumbo yao," anasema Joseph.

"Tofauti na binadamu au wanyama wengi, mamba hawezi kuvumilia kukaa kila bila kula muda mrefu, na kwa sababu hiyo, anaweza kukamata chochote ikiwa ni pamoja pia mamba wenzake," anasema Joseph.

Anasema kazi ya kumtunza mamba ni ngumu na inayohitaji umakini mkubwa, kwani kosa dogo tu anaweza kuua.

"Mamba hachagui nyama, kwake chochote kinachoitwa nyama ni halali yake, kuanzia ndege, mijusi, samaki na hata binadamu, sasa unapo muhudumia kwa kumpa chakula au kusafisha banda lao lazima kuwa makini sana."

Joseph anasema mamba anakula mara moja tu kwa wiki, na mkubwa anamaliza kilo kati ya 20 mpaka 25 za nyama, huku wengine wakila pungufu ya hapo kutegemeana na maumbo yao, na wadogo zaidi wenye miezi miwili au pungufu, husagiwa nyama na kulishwa mara mbili kwa wiki.

Anasema Mamba anaweza kufahamika umri wake kwa kuangalia mambo mengi, lakini namna magamba ya ngozi yake yanavyoonekana ni moja ya njia hizo.
Kitabia, anasema mamba dume na jike wote hupevuka wanapofika umri wa miaka 15 na kipindi hicho ndipo wanapoanza kujamiiana, kisha kutaga mayai ambapo kwa wastani jike anaweza kuanza kutaga kati ya mayai 30-50.

"Tabia za jike anapokuwa tayari kujamiiana huwa hatulii na mara zote husumbua madume ikiwa ni ishara ya kuwa anahitaji kupandwa na hufanya tendo hilo wanapokuwa ndani ya maji tu," anasema Joseph.

Anasema mamba anaowafuga huwakamata mto Pangani, Wami na Ruvu na hufanya hivyo baada ya kupata kibali kutoka Maliasili.

"Kinachofanyika ni kwamba, sehemu ambazo mamba wanaonekana kuwa wengi katika mito hiyo, Maliasili hutupa kibali cha kwenda kuvuna kwa idadi itakayoelezwa," anasema Joseph.
 

No comments: