Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, April 29, 2012

Waathirika mabomu ya Mbagala wailalamikia Serikali

WAATHIRIKA zaidi ya 2,200, wa milipuko ya mabomu iliotokea Mbagala mwaka 2009 wameilalamikia Serikali kwa kushindwa kuwalipa fidia zao huku wakieleza kwamba bado wanaendelea kuishi katika mahema bila kupata msaada wowote.

Waathirika hao ambao jana walikusanyika katika Ofisi za Serikali ya Mtaa Mbagala Kuu Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam walisema kwamba licha ya kufanya jitihada mbalimbali za kudai haki zao ikiwa pamoja na kwenda kumuona Waziri Mkuu wameshindwa kupata msaada wowote tofauti na walivyoahidiwa pindi milipuko hiyo ilipotokea.

Mwenyekiti wa waathirika hao, Steven Gimange alisema tangu mwaka 2009 milipuko hiyo ilivyotokea hakuna msaada walioupata kwani bado wanaendelea kuishi katika mahema huku watu ambao waliathiriwa afya zao hakuna matibabu yoyote waliyoyapata, jambo ambalo limewaletea ulemavu wa viungo vya mwili.

Alisema Aprili 23 mwaka huu walienda kuonana na Waziri Mkuu ambapo  walipewa majibu ya kutorizisha jambo ambalo limewafanya waone kama sio watanzania kwani  wameshasahaulika na hawana haki tena.

“Baada ya kuona haki zetu za msingi zinataka kupotea tuliamua kwenda kuonana na Waziri Mkuu lakini cha kushangaza ni kwamba tuliambiwa suala la watu waliothirika na mabomu Mbagala limeshafungwa na halina mjadala tena,” alisema Gimange.

Mwenyeki huyo alibainisha kwamba licha ya kufanya jitihada hizo waliandika barua kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), ili waende kuwatembelea  na kufanya uchunguzi wa fedha zilizotolewa kwa ajili ya fidia zao kwani waliamini hawakutendewa haki katika malipo ya fidia zao.

Baadhi ya waathrika hao wakizungumza na mwandishi wa habari hizi walisema kwamba inasikitisha kuona wao ambao ndio walikua watu wa kwanza kupatwa na matatizo ya mabomu mpaka sasa bado hawajalipwa fidia zao licha ya kufanya jitihada mbalimbali za  kutafuta haki zao bila mafanikio.

Raurent Njige alisema kwamba kuna watu ambao walilipwa Sh30,000 huku wakiwa wamebomokewa na nyumba zao kabisa jambo ambalo nilakusikitisha kwani kuna baadhi ya watu wametumia tatizo hilo kujinufaisha wao wenyewe huku wao wakiendelea kuteseka.

No comments: