Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, June 8, 2014

Tuzo ya Nelson Mandela yaanzishwa na UN

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limeafiki kuanzishwa kwa tuzo ya Nelson Mandela kutokana na msimamo wake katika kusaka haki na usawa kwa wote.
Tuzo hiyo inalenga kuendeleza kazi aliyoitetea Mandela ya usawa wa binadamu na haki zao kwa kuwatia moyo wale wanaosimamia misingi hiyo ambayo pia Umoja wa Mataifa unazingatia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema hiyo ni hatua nyingine zaidi ya Umoja wa Mataifa kusongesha mbele kile ambacho Hayati Mzee Mandela alikiamini.
Mwakilishi wa kudumu wa Afrika Kusini kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Kingsley Mamabolo ametoa shukrani zake kufuatia uamuzi huo. Ameongeza kuwa kwa kuridhia azimio kuhusu tuzo ya Mandela, Umoja wa Mataifa umedhihirisha shukrani zake kwa dhima ongozi ya Mandela kwenye harakati za ukombozi wa Afrika na Umoja wa Afrika. Shujaa Nelson Mandela, Rais wa zamani wa Afrika Kusini na ambaye aliongoza mapambano ya miaka mingi dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, alifariki dunia Desemba mwaka jana akiwa na umri wa miaka 95.Shujaa huyo wa Afrika anaendelea kukumbukwa kwa jinsi alivyojitolea kwa ajili ya ukombozi wa watu wake na ataendelea kuwa kigezo kizuri cha ukombozi na kupigania haki.

No comments: