Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Friday, May 23, 2014

Jeshi la DRC latuhumiwa kuvunja haki za binaadamu

Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binaadamu, limewatuhumu askari wa usalama wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuvunja haki za binaadamu nchini humo. Shirikisho hilo limesema hayo wakati likitoa ripoti ya uchunguzi uliofanywa kuhusiana na matukio ya tarehe 30 mwezi Disemba mwaka jana nchini Congo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo askari wa usalama wa serikali ya Kinshasa, walitenda vitendo vilivyo dhidi ya haki za binaadamu, wakati wa kukabiliana na wanamgambo wa Kikristo wafuasi wa Askofu Paul Joseph Mukungubila Mutombo.
Taasisi hiyo ya haki za binaadamu imesema, katika operesheni za kuyakomboa maeneo kadhaa yaliyokuwa yametekwa na wanamgambo wa askofu huyo na licha ya kwamba wanamgambo hao walikuwa wamebebea fimbo na miti mikononi mwao, waliuliwa kikatili na askari hao wa serikali. Ripoti imefafanua zaidi kwamba, katika tukio hilo watu 103 waliuawa na askari hao wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hata hivyo taasisi hiyo imesema kuwa wahanga wa tukio hilo ni zaidi ya watu hao 103. Aidha imesema kuwa, baadhi ya wanachama wa askofu Mukungubila waliotiwa mbaroni hadi sasa wanaendelea kuadhibiwa kwa mateso makali ndani ya jela za nchi hiyo. Askofu Mukungubila Mutombo, alitiwa mbaroni katikati ya mwezi huu huko nchini Afrika Kusini.

No comments: