Serikali ya Misri iliyowekwa madarakani
kwa mapinduzi ya kijeshi imeitangaza Ikhwanul Muslimin kuwa ni kundi la
kigaidi, katika hatua ya utekelezaji ramani ya njia iliyoandaliwa tangu
yalipofanyika mapinduzi hayo dhidi ya Muhammad Morsi, rais halali wa
nchi hiyo. Mnamo siku ya Jumanne ya tarehe 24 mwezi huu, gari moja
lililotegwa bomu liliripuka kwenye kituo cha polisi cha mji wa Mansoura
kaskazini mwa mji mkuu wa Misri, Cairo na kusababisha vifo vya watu
wasiopungua 15 na kuwajeruhi makumi ya wengine. Muda mfupi baada ya
mripuko huo Sharif Shaufi, msemaji wa Waziri Mkuu wa Misri Hazim al
Beblawi, aliitangaza Ikhwanul Muslimin kuwa ni kundi la kigaidi.
Akimnukuu Waziri Mkuu huyo wa Misri Shaufi alidai kwamba kundi la Ikhwan
limeonyesha sura yake chafu ya kigaidi kwa kumwaga damu na kuvuruga
usalama wa Misri.
Hakuna asiyejua kwamba katika kipindi
chote cha miaka 85 tangu kuasisiwa kwake harakati ya Kiislamu ya
Ikhwanul Muslimin haijawahi kuuweka ugaidi katika ajenda ya utekelezaji
wa ratiba na mipango yake. Kwa muda wote huo wa zaidi ya miongo minane,
kwa mara kadhaa Ikhwanul Muslimin imepigwa marufuku na tawala tofauti za
Misri, lakini haijawahi hata mara moja kufanya vitendo vya kigaidi na
vya uripuaji mabomu au hata utumiaji nguvu dhidi ya tawala hizo. Kwa
maana hiyo basi, ikiwa mripuko wa siku ya Jumanne uliotokea Mansoura
hautokuwa umepangwa na serikali yenyewe ya muda ya Misri kwa lengo la
kuionyesha Ikhwan kuwa ni harakati inayofanya vitendo vya kikatili ili
kuweza kuifuta, basi utakuwa umetumiwa na serikali hiyo kama kisingizio
cha kutimizia ndoto ambayo imekuwa nayo muda wote huu.
Muhammad Morsi, rais halali wa Misri
aliondolewa madarakani tarehe 3 Julai mwaka huu kupitia mapinduzi ya
kijeshi. Na kuanzia wakati huo ikaanza kampeni ya kuchukua hatua dhidi
ya viongozi na wanachama wa Ikhwanul Muslimin kwa kuwatia nguvuni na
kuwaweka korokoroni. Katika kuendeleza mkakati huo ulioratibiwa dhidi ya
Ikhwan, serikali ya muda ya Misri ilichukua hatua ya kuivunja harakati
hiyo. Katika awamu hii muhimu ya tatu, serikali hiyo imekamilisha
mkakati wa kuifuta kikamilifu Ikhwanul Muslimin kwa kuitangaza kuwa ni
kundi la kigaidi.
Itakumbukwa kuwa baada ya kung'olewa
madarakani dikteta Hosni Mubarak, Ikhwanul Muslimin ilidhihirisha wazi
kuwa ndio harakati muhimu zaidi na yenye kupendwa zaidi na wananchi wa
Misri baada ya kujipatia ushindi wa kishindo katika chaguzi zote tatu za
kidemokrasia zilizofanyika nchini humo. Ni wazi kwamba hatua
iliyochukuliwa dhidi ya Ikhwan, lengo lake ni kuizuia harakati hiyo
muhimu isiwe na nafasi yoyote katika mazingira ya wakati huu ndani ya
jamii ya Misri ambapo nchi hiyo inajiandaa kwa kura ya maoni ya katiba
pamoja na uchaguzi wa rais na bunge. Kura ya maoni ya katiba mpya ambayo
imeandaliwa bila ya kuishirikisha Ikhwanul Muslimin imepangwa kufanyika
tarehe 14 na 15 za mwezi ujao wa Januari. Serikali ya mpito imekusudia
pia kuitisha chaguzi za urais na bunge baadaye mwakani, ambapo Waziri wa
Ulinzi Abdulfatah el Sisi aliyeongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya
Morsi ameonyesha nia ya kugombea katika uchaguzi ujao wa rais.
Majenerali wa jeshi na viongozi wa serikali ya mpito wametekeleza mpango
wa ramani yao ya njia wa kuifuta Ikhwanul Muslimin ili kuweza kuamua
juu ya mustakabali wa mfumo wa kisiasa wa Misri kwa urahisi zaidi na
pasina kukabiliwa na upinzani wowote wa kutia wasiwasi. Na lengo ni
kuhakikisha serikali ijayo ya Misri itakayofanya kazi kwa muongozo wa
wanajeshi si serikali ya mapinduzi ya kijeshi bali ni serikali
iliyopatikana kwa kura za wananchi hata kama ni kwa uchaguzi ambao
matokeo yake yalikwisha pangwa tangu kabla. Ili kufanikisha mkakati huo,
sambamba na kutangazwa Ikhwanul Muslimin kuwa ni kundi la kigaidi,
karibu vyama 30 na harakati kadhaa za kisiasa zimeasisi muungano uitwao
"Harakati ya Kitaifa" ya kuunga mkono ramani ya njia ya mustakabali wa
Misri pamoja na kuliunga mkono jeshi na polisi ya nchi hiyo. Lakini
nukta muhimu na ya kutaamali hapa ni kwamba serikali ya muda ya Misri
ilikitumia kisingizio cha mripuko wa bomu uliotokea siku ya Jumanne
kwenye kituo cha polisi mjini Mansoura kuitangaza Ikhwanul Muslimin kuwa
ni kundi la kigaidi, ilhali harakati hiyo ilitoa tamko rasmi la kulaani
shambulio hilo, na badala yake kundi linalojiita Ansaru Baitul Maqdis
likatoa taarifa siku ya Jumatano na kutangaza rasmi kuwa ndilo
lililohusika na shambulio hilo








No comments:
Post a Comment