Kikao cha Tano cha Mawaziri wa Maji wa Nchi za Kiarabu, kimefanyika
mjini Cairo Misri, kwa minajili ya kujadili tatizo la kupungua maji
katika nchi hizo. Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za Jumuiya ya
Nchi za Kiarabu (Arab League) mjini humo. Akizungumza katika kikao
hicho, Nabil al Arabi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema
kuwa, kuna changamoto nyingi mbalimbali zinazozikabili nchi wanachama,
kuhusiana na uga wa kuhifadhi maji yanayohitajiwa na nchi za hizo za
Kiarabu, hasa kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa na ukame wa muda
mrefu katika baadhi ya nchi hizo. Nabil al Arabi amesisitizia udharura
wa kuwepo mashirikiano makubwa kati ya nchi za Kiarabu,
kwa ajili ya
kutatua migogoro inayotokana na ukosefu wa maji na ukame. Ameongeza
kuwa, suala la kudhamini maji ni miongoni mwa masuala muhimu ya maisha
na kuzitaka nchi hizo kuimarisha mashirikiano. Hatua hiyo, inakuja ikiwa
ni baada ya kujiri suutafahumu kati ya nchi za Misri na Ethiopia
kuhusiana na matumizi ya maji ya Mto Nile. Wakati huo huo Mshauri wa
Rais wa Misri wa masuala ya kisiasa amesema kuwa, nchi hiyo itaitaka
Ethiopia kuacha kujenga bwawa katika mto wa Blue Nile, na kuongeza kuwa,
Misri ina hofu kuwa ujenzi huo utapunguza fungu lake la maji kutoka mto
huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)







No comments:
Post a Comment