Wakati zimesalia siku 19 kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais nchini
Zimbabwe na huku kampeni za uchaguzi huo zikipamba moto, Morgan
Tsvangirai, Waziri Mkuu wa Zimbabwe na kiongozi wa chama cha MDC
ameiandikia barua Jumuiya ya Ustawi ya Kusini mwa Africa SADC
akilalamikia maamuzi yaliyochukuliwa hivi karibuni na Rais Robert Mugabe
wa nchi hiyo ya kufanyika uchaguzi wa rais tarehe 31 Julai mwaka huu.
Tsvangirai amesema kuwa, uchaguzi huo utakuwa si wa kisheria, huru na
wa haki iwapo utafanyika tarehe hiyo iliyopangwa na Rais Mugabe. Naye
Tendai Biti Waziri wa Fedha wa Zimbabwe na ambaye pia ni Katibu Mkuu wa
chama cha MDC amesema kuwa, hadi sasa hakuna hatua zozote
zilizochukuliwa za kufanyika marekebisho muhimu nchini humo.
Hivi karibuni wakuu wa SADC walikutana kwenye kikao cha dharura huko
Maputo mji mkuu wa Msumbiji, na kumtaka Rais Mugabe aakhirishe tarehe ya
uchaguzi iliyopangwa awali kwa wiki mbili zaidi, mapendekezo ambayo
yalipuuzwa na Rais Mugabe. Chama cha MDC kinataka yafanyike marekebisho
kwenye vyombo vya habari, kikosi cha usalama na jeshi la polisi, taasisi
ambazo zinadhibitiwa na Rais Mugabe wa Zimbabwe.







No comments:
Post a Comment