Dar es Salaam. Rais wa Marekani Barack Obama
amehitimisha ziara yake ya Afrika mapema leo, kwa kutembelea mradi wa
uzalishaji umeme wa Symbion Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake Ubungo, Rais Obama alielezea
jinsi mkakati wa serikali yake wa kuhakikisha Afrika inapata umeme
utakavyoboresha maisha ya wakazi wa bara hili.
Mapema leo asubuhi, Rais Obama aliungana na Rais
wa zamani wa Marekani George Bush kuweka shada la maua kuwakumbuka
wahanga wa shambulizi la kigaidi la ubalozi wa Marekani mwaka 1998.
Katika ziara yake ya siku mbili iliyoanza jana
nchini Tanzania, Rais Obama amesisitiza umuhimu wa kuboshesha mahusiano
ya kibiashara kati ya Afrika na Marekani.
Marekani itaisaidia serikali ya Kikwete kuboresha
miradi mbalimbali ya umeme, miundombinu ya barabara, maji na programu za
kielimu kwa vijana kwa lengo la kuongeza ajira.
Jijini Dar es salama, Barabara za Ally Hassan
Mwinyi, Mandela, Sam Nujoma na ile ya Morogoro zilifungwa kwa muda
kuanzia majira ya saa tatu asubuhi huku maelfu ya wananchi wakitanda
barabarani kwa lengo la kumuaga rais huyo.
Mara baada ya kufika katika uwanja wa Ndege Rais
Obama na Mkewe walitumia muda mfupi kuagana na mwenyeji wao Rais
Kikwete na mkewe ikiwa ni pamoja na kuwaaga mamia ya viongozi waliofika
uwanjani hapo.
Mikakati ya Marekani Afrika
Kiongozi huyo aliwasili Dar es Salaam jana
mchana ikiwa ni nchi ya mwisho katika ziara yake barani Afrika
ikitanguliwa na Senegal na Afrika Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na Rais
Jakaya Kikwete Ikulu, Rais Obama alisema aliainisha mambo hayo wakati
alipozungumza na mwenyeji wake huyo.
Alisema katika mazungumzo hayo, waligusia mradi wa
mkubwa wa umeme uitwao Power Afrika wenye lengo la kuongeza kiwango cha
umeme kinachozalishwa nchini na barani Afrika ili kupata umeme nafuu na
wa uhakika utakaochagiza kuongeza uzalishaji na kukuza ajira.
Nchi nyingine za Afrika ambazo zitanufaika na mpango huo ni Kenya, Ghana, Liberia, Nigeria na Ethiopia.
Rais Obama alisema pia wamezungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo, ukuzaji wa demokrasia na utawala bora.
Alimzungumzia pia mchezaji nyota wa mpira wa
kikapu wa Tanzania, Hashimu Thabeet anayecheza katika Ligi Kuu ya
Marekani (NBA), akiwa na timu ya Oklahoma Thunder ya Marekani, akisema
hawakuzungumzia suala lake na kuahidi kufanya hivyo siku nyingine.
Akijibu swali iwapo anaridhishwa na misaada ambayo
nchi yake inatoa kwa Tanzania, Rais Obama alisema anafarijika kwa
matunda yanayopatikana katika mapambano dhidi ya malaria, barabara mpya
zinazojengwa na katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Hatutoi dawa, bali tunajenga miundombinu ya afya,
hatutoi chakula, bali kuwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula pia
tunasisitiza kubadilishwa kwa sheria mbalimbali ili kutoa fursa kwa
sekta binafsi kuleta mitaji yao kwa wingi zaidi, lakini jambo la muhimu
ni kuijenga Afrika,” alisema.
Kuhusu sekta ya utalii, Rais Obama alisema
watatangaza vivutio vya Tanzania, lakini kwa kuwa ameambiwa ujangili ni
tatizo, Serikali yake itaisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto
hiyo.
“Tutatangaza utalii, nimeelezwa ujangili ni tatizo
hivyo Marekani itasaidia kupambana na changamoto hiyo na tutaongeza
fedha kuhakikisha hali hiyo inatokomea,” alisema.
Akichangia hoja ya misaada ya Marekani, Rais
Kikwete alisema Mradi wa Maendeleo ya Changamoto za Milenia (MCC),
umekuwa msaada mkubwa kwa Tanzania.
Alisema kupitia MCC, Tanzania imepata msaada wa
kujengewa barabara katika maeneo ya vijijini na yale yanayozalisha
chakula kwa wingi.
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yamenufaika kwa
barabara hizo kuwa ni Namtumbo, Songea, Mbinga, Tunduma, Horohoro,
Tanga na baadhi katika Kisiwa cha Pemba.
Alisema Tanzania pia imenufaika kwa mradi wa maji
jijini Dar es Salaam ambao ujenzi wake unaendelea na umeme kwa ajili ya
maeneo ya vijijini ambao pia unafadhiliwa na Marekani katika mikoa 10 ya
Tanzania.
“Kusema kweli Marekani imefanya makubwa, nikisema
inatosha, Mheshimiwa Rais hatasikiliza maombi yangu mengine,” alisema
Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema kutokana na misaada ya Marekani, maambukizo
ya Ukimwi yamepungua, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua
na wale wanaozaliwa na wakiwa na VVU wamepungua kwa kiwango kikubwa.
Alisema pia Watanzania wamenufaika na msaada wa
vitabu milioni mbili vya sayansi. Alitumia fursa hiyo kuomba idadi
nyingine kama hiyo.
“Nimemwambia tunaomba vitabu vingine milioni mbili
na yeye akasema niongee na watu wake, lakini nilipowatazama nikaona
nyuso zao zinakubaliana na Rais wao,” alisema Kikwete.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliulizwa
kuhusu kesi ya Mtanzania aliyeshtakiwa Marekani kwa kumtumikisha binti
wa Kitanzania na kushindwa kulipa faini na kusema analifahamu suala
hilo, lakini limemalizika kwa wahusika kulipwa.
Alisema binti aliyelalamika alichukuliwa na dada
yake kwenda kusomeshwa Marekani, lakini alipofika akatumikishwa kwa kazi
za ndani aliwashtaki dada yake na shemeji yake na mahakama ikawatoza
faini ya Dola milioni moja za Marekani.
Hata hivyo, alisema haikuwa rahisi kwa wadaiwa
kulipa faini hiyo kutokana uwezo wao mdogo, kama ilivyo kwa Watanzania
walio wengi, hivyo waliomba faini ipunguzwe na ilipopunguzwa ikalipwa na
suala hilo likamalizika.
Aimwagia Tanzania Sifa
Akiizungumzia Tanzania, Obama alisema, “Hii ni
mara yangu ya kwanza kufika Tanzania, mzee wangu alikuwa Afrika
Mashariki na wakati fulani aliishi Tanzania, mke wangu na watoto wangu
wamefurahi kufika hapa.”
Alisema alipoingia madarakani Rais wa kwanza
kutoka Afrika kukutana naye alikuwa ni Rais Kikwete kwa kuwa Tanzania
inaheshimu utawala wa kidemokrasia.
Obama alisema Tanzania imefanya kazi nzuri pamoja
na Zanzibar kwa kufanikisha suala la Katiba Mpya kwa ajili ya Tanzania
ijayo kwani hiyo ndiyo demokrasia.
Pia aliipongeza Tanzania kuhusu hatua yake katika
kulinda amani katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na
Sudan hasa eneo la Darfur.
Alisema DRC inaathiriwa na machafuko kutokana na
kuwa na maliasili nyingi na kusema Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila na
watu wake wanahitaji kufanya kazi kubwa kuhakikisha amani inakuwapo.







No comments:
Post a Comment