Jeshi la Misri limetangaza kuwa, taarifa iliyotolewa jana kwa makundi
ya kisiasa ya kuyataka yafikie mwafaka, haina maana ya kutaka kufanya
mapinduzi ya kijeshi nchini humo.
Jeshi la Misri limeeleza kuwa, taarifa hiyo imetolewa kwa lengo la
kuyashinikiza makundi ya kisiasa na wanasiasa nchini humo kufikia
mwafaka na serikali ya Cairo. Taarifa hiyo imeeleza kuwa, iwapo
wanasiasa wa Misri watashindwa kufikia mwafaka na kutekeleza matakwa ya
wananchi katika kipindi cha masaa 48 yajayo, litalazimika kuingilia kati
kwa shabaha ya kutatua mgogoro huo.
Wakati huohuo, masaa machache baada ya jeshi kutoa muda wa masaa 48
ya kutatuliwa mgogoro wa Misri, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Misri
Muhammad Kamil Amr ametangaza kujiuzulu, baada ya kushadidi maandamano
ya wapinzani wa Rais Morsi. Hadi sasa mawaziri 10 na magavana watatu wa
serikali ya Misri wameshajiuzulu. Vilevile mshauri wa masuala ya kijeshi
wa Rais Morsi naye alitangaza kujiuzulu hapo jana.







No comments:
Post a Comment