Kuongezeka vitendo vya ukandamizaji dhidi ya Waislamu nchini
Ufaransa kumeendelea kulaaniwa na kukosolewa na jamii ya Waislamu sio tu
nchini humo bali pia katika bara zima la Ulaya. Radiamali ya Waislamu
wa Ulaya kwa vitendo vya chuki dhidi ya dini yao Tukufu huko Ufaransa ni
dhihirisho la kukerwa kwao na jinsi mizizi ya fitina na chuki dhidi ya
Uislamu inavyozidi kusambaa kwa kasi katika bara hilo. Ni kutokana na
hali hiyo, ndiyo maana Waislamu nchini Uingereza wakaandaa maandamano
makubwa kulalamikia vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu ndani na nje ya
Uingereza.
Waandalizi wa maandamano hayo wamesema mara hii walikwenda
mpaka ofisini kwa Waziri Mkuu, David Cameron kuwasilisha rasmi
malalamiko yao.
Katika siku za hivi karibuni na tangu kutokea shambulizi dhidi ya
ofisi za jarida la kila wiki la Cherlie Hebdo nchini Ufaransa mwanzoni
mwa mwezi uliopita, ukandamizaji, udhalilishaji na chuki dhidi ya
Uislamu vimeongezeka maradufu barani Ulaya. Jarida hilo mara kadhaa
limekuwa likimvunjia heshima Mtume Mtukufu, Muhammad SAW kwa kumsawiri
kupitia vibonzo. Licha ya Waislamu kukosoa na kulaani udhalilishaji huo,
viongozi wa Ulaya wamekuwa wakisisitiza kuwa hawawezi kuingilia kadhia
hiyo kwani jarida lenye kufurutu ada la Charlie Hebdo linatumia uhuru
wake wa kujieleza. Baraza la kupambana na hofu na chuki dhidi ya Uislamu
(Islamaphobia) nchini Ufaransa limesema tangu watu wenye silaha wavamie
ofisi za Cherlie Hebdo Januari 7 mwaka huu, kumeshuhudiwa zaidi ya visa
50 vya uvamizi na ukandamizaji dhidi ya Waislamu.
Nchini Ujerumani nako, makundi yanayoeneza propaganda chafu na chuki
dhidi ya Uislamu yamezidi kupata nguvu; na inavyoonekana, wimbi jipya la
harakati hiyo linazidi kuibuka na kuenea kote barani Ulaya. Hata hivyo,
kusimama kidete Waislamu wa Ulaya kumezuia kwa kiwango fulani, kasi ya
kuenea harakati hizo. Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani linasema
kuwa, wanawake Waislamu wenye kuvaa hijabu pamoja na mashekhe wenye kuva
kofia na vilemba wamekuwa wakisumbuliwa na kunyanyaswa na makundi ya
Wakristo yenye kufurutu ada katika miezi ya hivi karibuni. Baraza hilo
pia limesema takriban kila wiki misikiti hushambuliwa ima kwa mawe au
kwa mabomu ya petroli na vijana wa makundi yanayoeneza chuki dhidi ya
Uislamu.
Ni mazingira kama hayo yanayowafanya Waislamu wa barani Ulaya
kuingiwa na wasiwasi zaidi siku baada ya siku. Hii ni katika hali
ambayo, serikali za nchi za Ulaya badala ya kulishughulikia tatizo la
chuki na hofu dhidi ya Uislamu (Islamaphobia) na kulipatia ufumbuzi,
wamebaki kimya; na wanapozungumza wanatumia visingizio kama shambulizi
dhidi ya jarida la Charlie Hebdo kuhalalisha uafiriti unaofanywa na raia
wao dhidi ya jamii ya Waislamu.







No comments:
Post a Comment