Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid al Muallem, amesema kuwa irada ya
wananchi wa Syria ndiyo pekee itakayoweza kuainisha mustakbali wa nchi
hiyo. Al Muallem ameyasema hayo leo baada ya kushiriki katika uchaguzi
wa rais wa nchi hiyo na kuongeza kuwa, kujitokeza kwa wingi sana
wananchi katika uchaguzi wa leo wa kidemokrasia na huru, kutaainisha
mustakbali wa taifa hilo.
Amesema, Wasyria wameshiriki katika uchaguzi
huo kwa uhuru na kwamba, serikali ya Damascus inawapa umuhimu mkubwa
wananchi kwani ni wananchi hao ndio wenye haki ya kuchagua mfumo
wanaoutaka. Amesisitiza kuwa, hivi karibuni ulimwengu utashuhudia
kushindwa njama za maadui wa taifa hilo. Ameusifu ushiriki mkubwa wa
wananchi katika uchaguzi wa leo na kusema kuwa, uchaguzi huo utaandaa
mazingira ya amani, utulivu, ujenzi mpya wa nchi na kutatuliwa kisiasa
mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu. Kwa upande mwingine amekusifu kusimama
kidete na muqawama wa taifa hilo dhidi ya njama na hila za maadui
wasioitakia mema Syria. Rais Bashar al-Assad wa Syria amepiga kura
katika kituo cha kupigia kura cha eneo la Hayyu al-Maliki mjini
Damascus, huku Hassan Abdullah al Nouri, mgombea mwengine wa nafasi hiyo
akipiga kura katika moja ya vituo vilivyowekwa katika hoteli ya
Sheraton mjini Damascus, ambapo pamoja na mambo mengine alisisitiza
kuwa, uchaguzi huo ni wa kidemokrasia na huru. Zaidi ya watu milioni 15
waliotimiza masharti ya kupiga kura wameshiriki kwa katika uchaguzi wa
leo. Wakati huo huo Spika wa bunge la Syria, Mohammad Jihad Al-Liham,
amesema kuwa, ushiriki mkubwa wa Wasyria katika uchaguzi wa leo
umewashangaza walimwengu. Uchaguzi wa rais nchini Syria umefanyika
katika mikoa yote ya nchi hiyo, ispokuwa mkoa wa al-Riqqah ambao
unadhibitiwa na magenge ya kigaidi.







No comments:
Post a Comment