Watu wasiopungua 37 wameuawa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo katika hujuma ambayo imetajwa kuwa ni ulipizaji kisasi kufuatia
wizi wa ng'ombe. Tukio hilo limejiri jana Jumamosi katika kijiji kimoja
mkoani Kivu Kaskazini na imearifiwa kuwa kati ya waliopoteza maisha ni
mwanamke na watoto ambao walipigwa risasi na kudungwa visi au kuchomwa
moto ndani ya nyumba zao.
Baadhi pia wameuawa wakiwa ndani ya kanisa
kijijini hapo walipokuwa wakikimbilia hifadhi. Waathirika wote wa hujuma
hiyo ni wa kabila la Bafuliru. Bado haijabainika ni nani hasa
aliyetekeleza hujuma hiyo lakini kwa muda sasa kumekuwepo na mzozo baina
ya watu wa kabila la Bafuliru na Warundi wanaoishi katika eneo hilo.
Gavana wa Kivu Kusini Marcellin Cishambo amethibitisha kuwa mgogoro huo
ulikuwa wa mifugo na kuongeza kuwa tatizo kubwa ni kwamba karibu kila
mtu ana silaha katika eneo hilo.
Eneo la mashariki mwa DRC limekuwa likikumbwa na machafuko ya mara kwa mara tokea mwaka 1998.







No comments:
Post a Comment