Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Sunday, April 14, 2013

Tatizo kubwa la virusi sugu leo limetokana na utoaji dawa kali kiholela...

Enzi hizo hatukua na Ukimwi.
Magonjwa ya zinaa hayakuua mtu. Dalili yake ilikuwa kuwashwa na kujisikia vibaya wakati wa kwenda haja ndogo tu, basi.  Yakikuzidia  unazunguka zunguka mitaani unanunua dawa  rangi mbili- kidonge cha “tetracylene”- aghali ndiyo; lakini kinamaliza kabisa tatizo. Baadaye miaka ya themanini Ukimwi ukatangaza ufalme. Ukimwi haukuponywa kwa kidonge kama hicho. Na hata baada ya miaka thelathini, Ukimwi ulipoanza kutibika katika nchi zilizoendelea, haikua kidonge kimoja, bali ni vingi.  Tena bei yake si ya porojo. Sijasikia mtu anayeweza kuingia tu sehemu akanunua msururu wa vidonge vya kutibu Ukimwi. Tiba hii ilihimili, lakini haijaondoa kirusi, abadan.
Kawaida kirusi cha Ukimwi huwa kinamshinda mwanadamu kwa vile hushambulia mfumo mzima wa “kinga maradhi” mwilini.  Ingekuwa kirusi hiki hushambulia tu, ingetosha kuzuilika kama ambavyo virusi vingine huzuilika, kule kubadilika badilika kwake ndiyo kiini cha  zogo. Ndiyo maana Waswahili tulivyo wabunifu tukaukatia ugonjwa majina kama ‘ngoma’, ‘bomu’  ‘mdudu,’n a kadhalika.

Lakini watafiti  hawajalala. Karibuni wametangaza kuanza kuelewa namna Kirusi cha Ukimwi kinavyotekeleza ufisi wake. Waganga hao Dk Barton Haynes na John Mascola  walifanya majaribio kwa mgonjwa wa Ukimwi kutoka Afrika na kuchora ramani (“mapping”) ya mwenendo mzima. Hatimaye, tiba iko karibu ndivyo jarida la VR-Zone.Com  la Marekani lilivyotangaza kwa hamasa juma lililopita.
Hoja niliyoieleza hapa inaonyesha namna matangazo ya tiba za magonjwa mbalimbali zinazowasakama wanadamu yalivyo muhimu.
Mbali na Ukimwi yapo maradhi yenye virusi vikali,yanayoendelea kutusakama wanadamu, mathalan- Malaria, Saratani na Kifua Kikuu kilichoanzakurejea karibuni...
Tatizo haliko katika haya maradhi bali katika sugu, ambayo virusi vimejenga. Sikilizeni kisa kifupi.
Takriban miaka 15 iliyopita nilipohamia hapa Uingereza niliwahi kwenda zahanati ndogo ya kitongoji ninachoishi shauri ya mafua makali. Kawaida mafua ni ugonjwa katili sana jamii hizi za nchi baridi , huja majira yanapobadilika  mwezi Mei  kutoka msimu wa baridi kuingia joto na Novemba ambapo joto kuisha na kipupwe kuanza. Kufika kwa mganga akanipima presha, moyo, pumzi naye akasema niko sawa kabisa.
“Lakini daktari silali, usiku kucha napiga chafya.”
Akaniangalia kwa macho yenye mseto wa  huruma nacheko.
“Sikiliza. Wewe mzima kabisa bwa’ mkubwa; moyo na mwili wako viko shwari shauri unafanya mazoezi, unajiangalia; huvuti sigara,unajali unachokula, afya yako kama ya kijana wa miaka 20 (nilikua na miaka arobaini). Nenda zako tu nyumbani kapumzike. Usitoke toke; kunywa maji kwa wingi, lala kwa muda mrefu. Utapona tu.”
Duu, nikamwona mganga yule ambaye aliwahi pia kufanya kazi Tanzania kama ana mipango mibaya nami.
“Naomba unipe dawa kali daktari. Siwezi nikakaa nyumbani na mafua, bila dawa yeyote. Unajua mafua yanaua hapa kwenu Ulaya?”
Akacheka.
“Nimeifanya kazi hii karibu miaka 30. Usipende sana kunywa kunywa dawa. Nenda zako tu nyumbani kapumzike. Baada ya siku tatu ukiona hali mbaya rudi tena nitakupa hiyo dawa kali unayoitaka.”

No comments: