Vyama na harakati za upinzani nchini Bahrain vimetangaza kuwa utawala wa
Aal Khalifa hauna nia ya kuona mazungumzo ya nchi hiyo yanakuwa na
tija; na kwa sababu hiyo mazungumzo hayo yamegonga mwamba. Huku
vikibainisha kuwa utawala wa Aal Khalifa umevitumia vikao 20 vya
mazungumzo yaliyofanyika huko nyuma kwa ajili ya kupoteza muda na wala
haujajali na kuzingatia mitazamo na matakwa yao, vyama na harakati za
upinzani nchini Bahrain vimeeleza bayana kuwa lengo la utawala wa Manama
ni kukwamisha malengo ya mapinduzi, lakini wananchi wa Bahrain
wataendelea kuandamana kwa amani dhidi ya utawala wa Aal Khalifa hadi
watakapopata matilaba na matakwa yao. Jamil Kadhim, mwanaharakati wa
kisiasa nchini Bahrain amesema utawala wa ukoo wa Aal Khalifa unaendelea
kutia nguvuni watu, kuwafunga, kuwatesa, kuvamia nyumba na maeneo ya
kidini, kuwabagua na kutoa uraia kwa wageni ili kuvuruga muundo wa idadi
ya watu, na kwamba jinai hizo zinafanywa huku jamii ya kimataifa na
nchi za Kiarabu zikibaki kuwa watazamaji tu.
Khalil al Marzuq, Naibu
Katibu Mkuu wa harakati ya Kiislamu ya al Wifaq anayehusika na masuala
ya kisiasa amesisitiza juu ya ulazima wa kuhitimishwa dhulma na uonevu
nchini Bahrain. Al Marzuq amesema Bahrain haitokuwa tena mahala pa
kuendeleza dhulma na ukiritimba, kwa sababu mwenendo wa ukiritimba hauna
tija nyengine ghairi ya uharibifu na kwamba wananchi wa Bahrain
wameshaainisha njia wanayotaka kuifuata. Jawad Firuz, mwanaharakati wa
upinzani nchini Bahrain ameeleza kuwa utawala wa Aal Khalifa unavitumia
vyombo vya mahakama kama silaha ya kuwakandamizia wapinzani. Firuz,
ambaye ni mbunge wa zamani katika bunge la Bahrain ameiambia kanali ya
televisheni ya BBC ya Kiarabu kuwa jumuiya za kutetea haki za binadamu
zina mtazamo mmoja juu ya suala hili kwamba hukumu zote za mahakama za
Bahrain zinatolewa kwa lengo la kuwashinikiza kisiasa wanamapinduzi wa
nchi hiyo. Upinzani wa wanaharakati wa kisiasa kwa ukandamizaji
unaofanywa na utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain dhidi ya matakwa
halali ya wananchi unadhihirishwa katika hali ambayo watu saba
wamejeruhiwa katika mashambulio yanayoendelea kufanywa na vikosi vya
usalama vya utawala huo wa kifalme dhidi ya raia wa nchi hiyo. Kwa
mujibu wa kanali ya televisheni ya al Alam raia hao wamejeruhiwa katika
mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya usalama vya utawala wa Aal
Khalifa vikishirikiana na majeshi vamizi ya Saudi Arabia dhidi ya
waandamanaji katika maeneo ya Karazkan, Sitra na al Qaryah. Aidha raia
21 wametiwa nguvuni katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Tangu mwezi
Februari mwaka 2011 hadi sasa Bahrain inashuhudia maandamano ya amani ya
wananchi wanaopigania mageuzi; lakini hadi sasa mamia ya watu
wameshauawa na kujeruhiwa kutokana na ukandamizaji wa vikosi vya utawala
wa Aal Khalifa vikishirikiana na vile vya Aal Saudi. Kwa mujibu wa
nyaraka na ushahidi wa mashirika ya kutetea haki za binadamu wapinzani
kadhaa wa utawala wa Aal Khalifa wameuawa kutokana na mateso, na makumi
miongoni mwao wamebaki na vilema. Aidha akina mama kadhaa waja wazito
mimba zao zimeharibika kutokana na athari ya kuvuta gesi ya sumu
waliyopuliziwa na vikosi vya utawala wa Aal Khalifa katika maandamano ya
amani ya kuupinga utawala huo kandamizi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)







No comments:
Post a Comment