Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Saturday, April 28, 2012

El Baradei aunda chama kipya cha siasa Misri

Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki Muhammad El Baradei ameanzisha chama kipya cha siasa nchini Misri. El Baradei amesema chama hicho kipya kinaitwa "Katiba."
Akitangaza habari hiyo leo mjini Cairo Muhammad El Baradei amesema kuwa lengo la kuanzishwa chama hicho kipya ni kubuni katiba mpya ya kimapinduzi na kuitisha uchaguzi huru na wa haki.
Ameongeza kuwa sheria za Misri zinapaswa kuruhusu watu kupinga na kukosoa matokeo ya uchaguzi wa Rais na kwamba kifungu nambari 28 cha katiba ya muda ya nchi hiyo kinapaswa kufutwa.
Kwa mujibu wa kifungu hicho matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Misri hayawezi kupingwa au kutazamwa upya na malalamiko ya aina yoyote dhidi ya matokeo hayo hayatakubaliwa.
El Baradei pia amelikosoa Baraza Kuu la Kijeshi la Misri akisema kuwa utendaji wake umekuwa kinyume kabisa na matarajio ya Wamisri.
Baraza Kuu la kijeshi la Misri lilichukua madaraka ya nchi baada ya kung'olewa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak mapema mwaka 2011.

No comments: