Mahakama ya Katiba nchini Mali, imesema kuwa watu 36 ya
wameshajiandikisha kwa ajili ya kushiriki kwenye kinyang’anyiro cha
uchaguzi ujao wa rais nchini humo. Wanne kati ya watu hao
waliojiandikisha kugombea katika uchaguzi huo, ni mawaziri wakuu wa
zamani na mawaziri wawili wanawake ambao waliwahi kuwa wawakilishi
katika bunge la taifa hilo la magharibi mwa Afrika. Hii ni katika hali
ambayo, Tiébilé Dramé, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Mali ambaye
aliongoza ujumbe wa serikali ya mpito ya Bamako katika mazungumzo ya
kusaka amani na kundi la Tuareg linalopigania kujitenga eneo la Azawad
la kaskazini mwa Mali, huko mjini Ouagadougou, Burkinafaso, ni miongoni
mwa watu wenye nia ya kushiriki kwenye kinyang’anyiro hicho.
Mahakama ya
Katiba ya Mali itatangaza majina ya watu waliotimia masharti ya
kugombea tarehe 7 Julai mwaka huu sambamba na kuanza kampeni za uchaguzi
huo. Kwa mujibu wa wa muda ulioainishwa na serikali ya mpito ya
Bamako, uchaguzi wa rais unatakiwa ufanyike tarehe 28 mwezi huu wa
Julai huku duru ya pili ya uchaguzi huo ikiwa imepangwa kufanyika tarehe
18 Agosti mwaka huu ikiwa italazimu kufanya hivyo. Pamoja na hayo
Mamadou Diyamontin, Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo
amesema kuwa, kwa sasa ni vigumu kupatikana watu milioni nane
waliotimiza masharti ya kupiga kura katika uchaguzi huo. Hii ni kwa
sababu karibu raia laki tano wa nchi hiyo wamekuwa wakimbizi kutokana na
vita vya ndani. Aidha Diyamontin ameitaja hali ya ukosefu wa amani na
utulivu wa kisiasa nchini humo hususan katika mji wa Kidal wa kaskazini
mashariki wa nchi hiyo ambao hadi leo bado unadhibitiwa na waasi wa
Kituareg, kuwa ni sababu nyingine inayokwamisha kufanyika uchaguzi huo
wa rais. Pamoja na kuwepo makubaliano ya usitishaji vita kati ya
serikali ya mpito na makundi ya watu wenye silaha wa kabila hilo la
Tuareg, lakini hadi sasa bado majeshi ya nchi hiyo, yameshindwa kuingia
katika mji huo uliotajwa. Wakati huo huo, Harakati ya Taifa ya Ukombozi
ya Azawad ya kabila la Tuareg mjini Kidal, imesisitiza kuwa, hakuna
kizuizi chochote kitakachoweza kuzuia kufanyika uchaguzi huo mjini humo.
Baadhi ya duru zinatabiri kuwa, kufanyika uchaguzi katika hali ya
mivutano iliyopo hivi sasa nchini Mali, kutapelekea serikali
itakayochukua madaraka kutoka kwa utawala wa sasa wa mpito, kukosa
nguvu. Aidha wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kuwepo ujumbe wa vikosi
vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani nchini Mali kinachojulikana kwa
jina la MINUSMA, kutasaidia kufanikisha uchaguzi wa terehe 28 mwezi huu.
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wapatao 12600 ambao wengi
wao wanatoka nchi za Afrika, wanaanza operesheni yao hiyo hii leo
Jumatatu ya Julai Mosi. Imepangwa kuwa, vikosi hivyo vichukue jukumu la
kulinda usalama na amani huko kaskazini mwa Mali kutoka kwa askari wa
Ufaransa. Hivi sasa kuna askari 3,000 wa Ufaransa katika eneo hilo na
inasemekana kuwa idadi hiyo itapungua hadi askari 1,000 ifikapo mwishoni
mwa mwaka huu wa 2013.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment