Riek Machar kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini na makamu wa rais
wa zamani amesema kuwa, hana udhibiti kamili wa vikosi vya waasi ambavyo
vinatuhumiwa kuleta machafuko nchini humo. Akihojiwa na shirika la
habari la AFP mjini Nairobi nchini Kenya, Machar ameeleza kwamba,
itakuwa si kweli akisema kuwa anawadhibiti waasi wote lakini kwamba ana
matumaini ataweza kuwadhibiti kwani wamewapa mafunzo na miongozo.
Kiongozi huyo wa waasi wa Sudan Kusini aidha amesema, katika jeshi lao
kuna wapiganaji waliojitolea, ambao wana silaha zao wenyewe na
wamejiunga kwenye vita.
Mapigano yaliyojiri kati ya jeshi la Sudan Kusini na waasi watiifu
kwa Rieck Machar yamesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine
zaidi ya milioni 1.3 kuwa wakimbizi. Makubaliano ya kusitisha mapigano
yalifikiwa hivi karibuni kati ya pande hizo mbili huku mazungumzo ya
kusaka amani ya kudumu yakiendelea.







No comments:
Post a Comment