Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, April 3, 2012

Ecowas kujadili hali ya Mali

ECOWAS
Viongozi wa nchi wanachama katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za magharibi mwa Afrika ECOWAS walitazamiwa kukutana leo katika mji mkuu wa Senegal, Dakar kwa ajili ya kujadili hali ya mambo katika nchi jirani ya Mali.

Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast, Mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS ambaye yuko nchini Senegal kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za kuapishwa rais mpya wa nchi hiyo, ameelezea wasiwasi wake kuhusu mgogoro wa sasa wa Mali na kutangaza kuwa viongozi wa nchi za Magharibi mwa Afrika watalinda umoja wa ardhi ya Mali na wanatoa wito wa kusitishwa harakati za uasi huko kaskazini mwa nchi hiyo.
Nchi ya Mali imekumbwa na machafuko tangu baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo. Zaidi ya wiki moja iliyopita jeshi la Mali lilimpindua na kumuondoa madarakani Rais Amadou Toumani Tuore wa nchi hiyo kwa madai kwamba serikali yake imeonyesha udhaifu katika kukabiliana na waasi wa Kituareg.
Harakati za waasi hao zimezidisha hali mbaya katika eneo la magharibi mwa Afrika ambalo limekuwa likisumbuliwa na harakati za kundi la al Qaida.
Viongozi wa nchi za Magharibi mwa Afrika wamelaani mapinduzi ya Mali na utumiaji mabavu ulioiondoa madarakani serikali halali na wametoa wito wa kurejeshwa utawala wa katiba. Msemaji wa jumuiya ya ECOWAS amesema kuwa viongozi wa nchi wanachama wameafikiana juu ya suala la kutuma vikosi vya jeshi nchini Mali kwa ajili ya kukabiliana na waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo na kurejesha utulivu nchini humo.
Wakati huo huo waasi wa Kituareg wametumia hali ya machafuko inayotawala nchini Mali na kujiimarisha zaidi. Msemaji wa waasi hao amesema kuwa kundi hilo limetwaa miji muhimu ya Kidal, Gao na mji wa kihistoria wa Timbuktu. Hatua hiyo itawawezesha waasi wa Kituareg kudhibiti kirahisi maeneo yote ya kaskazini mwa Mali. Inaoneka kuwa jeshi la Mali ambalo lilitumia udhaifu wa Rais Amadou Toure katika kukabiliana na waasi wa Kituareg kama kisingizio cha kuiong'a madarakani serikali yake limeshindwa pia kupambana na waasi hao.
Kabila la Tuareg linaundwa na makundi ya jangwani yanayoishi katika maeneo ya mipaka ya nchi za Mali, Niger na Algeria. Waasi hao wanataka eneo hilo la kaskazini mwa Mali litangazwe kuwa eneo huru na mapato yanayotokana na madini ya eneo hilo yatumiwe katika eneo hilo hilo pekee. Eneo la kaskazini mwa Mali lina utajiri mkubwa wa mafuta na madini ambayo bado hayajachimbwa.

No comments: