Leo ni Jumatano tarehe Mosi ya mwezi Rajab mwaka 1433 Hijria mwafaka na tarehe 23 Mei mwaka 2012 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1376 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya riwaya alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume wa Uislamu SAW katika mji mtakatifu wa Madina. Imam Baqir AS aliishi katika zama za watawala madhalimu wa Bani Umayyah. Mtukufu huyo alishika hatamu za kuongoza umma wa Kislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Sajjad AS. ***
Leo ni tarehe Mosi ya mwezi Rajab, moja kati ya miezi yenye baraka na fadhila kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwezi huu na miezi miwili ijayo ya Shaaban na Ramadhan ni miezi ya mja kujitengeneza na kujikurubisha kwa Allah kwa ajili ya kuelekea kwenye ukamilifu na saada. Mtume SAW ameutaja mwezi huu kuwa ni mwezi mkubwa wa Mwenyezi Mungu, na ambao ndani yake imeharamishwa vita na makafiri. Mtume SAW amenukuliwa akisema, Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Shaaban ni mwezi wangu na Ramadhan ni mwezi wa umati wake. Kufunga suna katika mwezi huu kuna thawabu nyingi. Tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab kulitokea tukio kubwa katika historia ya Uislamu ambapo Mtume Muhammad alibaathiwa na kupewa Utume na tarehe 13 ya mwezi huu pia, alizaliwa Imam Ali bin Abi Talib AS. ****
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita mji wa Khoramshahr wa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Kiislamu na ukaondoka katika uvamizi wa majeshi vamizi ya Iraq. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane. Siku hii ya tarehe 3 Khordad inajulikana katika utamaduni wa mapinduzi ya Kiislamu kwa jina la "Siku ya Istiqama na Ushindi." ***
Na miaka 106 iliyopita na katika siku kama ya leo aliaga dunia Henrik Ibsen mwandishi wa tamthiliya wa nchini Norway. Alizaliwa mwaka 1828 kusini mwa Norway. Shauku na mapenzi ya Ibsen ya kuwa mwandishi wa tamthiliya ndiyo yaliyomsukuma kwenye taaluma hiyo. Mwandishi huyo wa Kinorway ameandika drama na tamthiliya nyingi. Moja kati ya tamthmliya zake mashuhuri ni ile iitwayo, An Enemy of the People yaani Adui wa Watu.
No comments:
Post a Comment