Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Friday, June 14, 2013

Kukiukwa haki za wafungwa katika jela za Saudi Arabia

Miongoni mwa changamoto zinazowakabili viongozi wa Saudi Arabia katika miaka ya hivi karibuni ni kukiukwa haki za wanawake. Kuhusiana na suala hilo, jambo ambalo limekuwa likiakisiwa zaidi na duru za habari katika siku za hivi karibuni ni kufichuliwa habari ya kuteswa wanawake katika jela za nchi hiyo. Wapinzani wa serikali ya Riyadh wamefichua kwamba, maafisa wa jela ya al Swafraa nchini Saudia wanawatesa wanawake wanaoshikiliwa kwenye jela hiyo.
Taarifa iliyosambazwa na wapinzani hao inaeleza kuwa, maafisa wa jela hiyo iliyoko katika mji wa al Barida, waliwalazimisha wafungwa 7 wa kike wa jela hiyo kutia saini makaratasi ambayo haikujulikana yameandikwa nini na kisha kuwatesa. Hii si mara ya kwanza kufichuliwa suala la kuteswa na kunyanyaswa wafungwa katika jela za Saudia hasa wanawake. Nchi hiyo ya Kiarabu inaongozwa kwa sheria zisizokuwa wazi. Watawala wa nchi hiyo ambao wengi wao ni wana wa Abdulaziz muasisi wa ukoo unaotawala wa Aali Saud, katika miaka ya hivi karibuni wameendelea kuitawala nchi hiyo kiimla. Katika nchi hiyo, kila sauti ya mpinzani huzimwa lakini pengine tunaweza kusema kuwa, wanawake wa Saudia ndio wanodhulimiwa zaidi. Hii ni kwa sababu hawana haki yoyote ya kiraia, na ni miongoni mwa masuala yanayopelekea watawala wa Riyadh kukosolewe sana. Amma suala lisiloweza kupingika ni hili kuwa, tangu kuanza harakati za kimapinduzi za wananchi wa Saudi Arabia, haki na uhuru wa kirai ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikikandamizwa kikamilifu na watawala wa Aali Saudi zimeanza kuzingatiwa na kuakisiwa zaidi. Miaka miwili na nusu imepita tangu harakati hizo zianze na katika kipindi chote hicho wanawake pia wamekuwa wakishirikiana bega kwa bega na wanaume katika kudai haki zao walizoporwa. Lakini watawala wa Riyadh badala ya kuzingatia matakwa hayo, wanakabiliana na wananchi kwa ukandamizaji. Katika miezi kadhaa iliyopita kumeripotiwa kuongezeka idadi ya wafungwa nchini humo hasa wanawake. Baadhi ya takwimu zinaonyesha kuwa, kuna wafungwa zaidi ya 30,000 nchini Saudia ambao mustakbali wa wengi wao haujulikani. Wafungwa hao wa kike na wa kiume wanakabiliwa na hali ya kusikitisha kama vile kushikiliwa muda mrefu bila kuhukumiwa na wakati huo huo kuteswa. Hali hiyo inathibitisha ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu nchini humo. Pamoja na hayo lakini hadi sasa hakuna taasisi yoyote ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu iliyochukua hatua ya kulaani na kukabiliana na hali hiyo. Kimya cha taasisi hizo kimepelekea watawala wa Aali Saudi wazidi kukiuka haki za binadamu, kuwakandamiza wananchi na kuendeleza siasa za kibabe nchini humo. Hata hivyo jambo hilo halijawavunja moyo wananchi wa Saudia na wanasisitiza kuendelea na harakati zao za kimapinduzi ili kuleta mabadiliko ya kisiasa na kudai haki zao muhimu zikiwemo za uhuru, demokrasia na kuondolewa ubaguzi katika jamii ya nchi hiyo. 

No comments: