Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Thursday, June 20, 2013

Alkhamisi, Juni 20, 2013

Leo ni Alkhamisi tarehe 11 Shaaban mwaka 1434 Hijria sawa na tarehe 20 Juni 2013 Miladia.
Miaka 1401 iliyopita katika siku kama ya leo mwaka 33 Hijria Qamaria alizaliwa mjini Madina Ali bin Hussein, mwana mkubwa wa Imam Hussein AS, Mjukuu wa Mtume Muhamad  SAW. Alishabihiana  sana na Mtume SAW na aliweza kunufaika kwa fadhila za maadila meme na maarifa ya Kiislamu kutoka kwa babu yake, Imam Ali AS na baba yake Imam Hussein AS. Kutokana na kuwa jina la Ali bin Hussein lilishabihiana sana na jina la ndugu yake mdogo ambaye pia alijulikana kama Ali, alipewa lakabu ya 'Ali Akbar' yaani Ali mkubwa. Alikuwa na nafasi kubwa katika harakati na mwamko wa baba yake mtukufu dhidi ya dhulma na utawala wa kiimala wa Bani Umayya.
Aliendeleza harakati hizo na katika siku ya tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria Qamaria, akiwa katika medani ya vita bega kwa bega na baba yake walipambana na jeshi katili ya Muawiyya huko Karbala na kwa ushujaa mkubwa aliuawa Shahidi.
@@
Miaka 101 iliyopita msomi wa Poland kwa jina la Casimir Funk kwa mara ya kwanza kabisa alifanikiwa kugundua vitamin au virutubisho. Baada ya uhakiki mwingi Daktari Casimir Funk aligundua kwamba vyakula vinavyotumiwa na mwanadamu vina baadhi ya virutubisho (vitamin) ambavyo japokuwa ni vichache sana lakini vina udharura mkubwa katika ukuaji na usalama wa mwili na akaamua kuvipa jina la Vitamini. Kuna anua ya vitamin kama vile , A,B, C, D, E na K na kila moja ina sifa na kazi maalumu katika mwili wa mwanaadamu.
@@@
Na siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 20 Juni 1973, Jose Domingo Peron mwanasiasa na muasisi wa Chama cha Peronist nchini Argentina, alirejea nchini mwake akitokea uhamishoni. Peron alikuwa afisa katika jeshi na alifanikiwa kuwa Rais wa Argentina mwaka 1946, na kufanya mabadiliko makubwa nchini humo. Hata hivyo udikteta wa Jose Domingo ulipunguza wafuasi wake na mwaka 1955 aliondolewa madarakani baada ya kufanyika mapinduzi. Lakini miezi michache baada ya kurejea kutoka uhamishoni Jose Domingo alifanikiwa kurejea tena madarakani na kuwa Rais wa Argentina. Mwaka mmoja baada ya kurejea madarakani Jose Domingo alifariki dunia, na mke wake Isabel Martines de Peron akawa Rais wa Argentina kuanzia mwaka 1974 hadi 1976.

No comments: