skip to main |
skip to sidebar
"Lowasa anahusika na kutekwa kwangu"-Nassari anena
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amemtuhumu
Mbunge wa Monduli Edward Lowassa kwamba anahusika na kipigo
alichokipata kutokana na chuki aliyonayo kwake.
Aidha amemtuhumu Spika wa Bunge, Anne Makinda kwamba naye ni
miongoni mwa watu wanaomchukia pamoja na viongozi wengine wa Bunge, kwa
kuwa hakuna kati yao aliyempigia simu au kumtumia ujumbe wa kumjulia
hali kutokana na kipigo alichopata ambacho kimemsababishia maumivu
makali.
Akizungumza jana akiwa kwenye chumba alicholazwa katika Taasisi ya
Tiba ya Magonjwa ya Mifupa na Ufahamu Muhimbili (Moi), Nassari alidai
Lowassa ambaye amewahi kuwa waziri mkuu kabla ya kujiuzulu, amemchukia
tangu alipomshinda mkwewe Sioi Sumari, kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge
uliofanyika Aprili mwaka jana.

Nassari aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Selian ya jijini
Arusha kabla ya kuhamishiwa MOI, alidai kupigwa na kuchaniwa nguo na
Green Guard wakati alipokuwa katika jitihada zake za kuhesabu kura
kwenye uchaguzi wa udiwani wa Kata ya Makuyuni-Monduli.
“Kipigo nilichopata Lowassa anahusika ananichukia, anataka
urais lakini hawezi kuupata kwa kuuumiza watu kama hivi, alifikiri
kwamba nitakufa sitakufa hadi kwa mapenzi ya Mungu,” alisema.
Alisema kuna jambo ambalo wananchi wanapaswa kulifikiria ni jinsi
ambavyo kumekuwa na matukio ya kutekwa na kuvamiwa, lakini hakuna
yanayohusisha kiongozi wa CCM, badala yake ni raia wa kawaida na
viongozi wa dini na siasa. Nassari alidai akiwa kama wakala mkuu wa
Chadema katika kata hiyo, alikumbana na mambo kadhaa yaliyomshangaza,
ikiwa ni pamoja na kufanyiwa jaribio la kutekwa mara mbili, kabla ya
kushambuliwa kwa kipigo.
Alisema pia anashukuru kwamba askari wawili waliokuwepo katika eneo
hilo walijitahidi kutaka kumnusuru, lakini walizidiwa nguvu na vijana
hao, hasa kutokana na kutokuwa na bunduki, ambapo yeye alipofanikiwa
kuchoropoka alikimbilia bastola yake na kuwanyoshea vijana hao bila
kufyatua.
Akizungumzia kuhusu hali yake, Nassari alisema amepimwa kipimo cha
X-ray ambapo imeonyesha kuwa pingili za mgongo wake zipo sawa, lakini
daktari ameshauri afanyiwe kipimo kingine kiitwacho MRI ili kuangalia
hali ya mishipa kutokana na maumivu makali anayoendelea kuyapata.
Aidha alitumia fursa hiyo kumshukuru Mbunge wa Kuteuliwa, Joseph
Mbatia kuwa ndiye aliyemsaidia kufanya mipango kuwasiliana na uongozi wa
Bunge na kumwezesha kuhamishiwa Moi, baada ya wabunge wote wa Chadema
kwenda Arusha kushughulikia waliofariki kwa bomu.
Hata hivyo, Lowassa alipotafutwa kuhusiana na tuhuma hizo alikataa
kuzungumzia suala hilo na kusema hilo aulizwe Msimamizi wa Uchaguzi,
Paulo Kitaleki.
Mwananchi ilimtafuta Kitaleki ambaye pia ni katibu tarafa, alikanusha
kuhusika kwa Lowassa akielezea kuwa siku ya tukio hilo alikuwa Geita.
“Huyu Nassari ni mwigizaji na anafaa kuwa msanii kwa kuwa
anaigiza tu hata hakupigwa, bali yeye ndiyo aliyempiga Wakala wa CCM,
Hussein Osama ambaye ni mlemavu, kisha akatimua mbio baada ya vijana
kutaka kumkamata, nashangaa kumwona yupo hospitali akidai kupigwa, siyo
kweli,” alisema Kitaleki.
No comments:
Post a Comment