
Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola
Uchaguzi wa Bunge na Rais wa Angola unatarajiwa kufanyika Agosti 31 mwaka huu. Kuna uwezekano mkubwa kwa Rais Jose Eduardo dos Santos kuendelea kuongoza nchini hiyo. Dos Santos anaongoza nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta kwa miaka 32 sasa. Taarifa zinasema kuwa, uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Baraza la Taifa, ambayo ni bodi ya ushauri yenye wajumbe 19 wakiwemo maafisa wa ngazi za juu wa serikali, viongozi wa upinzani na majaji kadhaa wa mahakama. Uchaguzi huo utakuwa ni wa pili kufanyika katika nchi hiyo ya pili kwa kuzalisha mafuta kwa wingi barani Afrika, tangu vilipomalizika vita vya miaka 27 vya wenyewe kwa wenyewe, mwaka 2002. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, chama cha MPLA cha Rais Dos Santos kilipata ushindi wa asilimia 82 ya kura katika uchaguzi wa 2008. Hivi sasa Dos Santos anahesabiwa kuwa ni mmoja wa viongozi waliokaa madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika baada ya yule wa Equatorial Guinea, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo. Licha ya kutangazwa tarehe ya uchaguzi, lakini bado kuna utata kati ya vyama vya upinzani kuhusu uhuru na uwazi wa uchaguzi huo. Chama cha MPLA kimekuwa kikitawala nchini humo tangu mwaka 1975 yaani tangu nchi hiyo ilipopata uhuru. Zoezi la kusimamia uandikishaji wapiga kura nalo limekabidhiwa shirika la kimataifa la Deloitte jambo ambalo wapinzani wanasema ni ukiukaji wa wazi wa sheria za uchaguzi. Wapinzani hao wanalalamika kuwa serikali ina ushawishi mkubwa katika shirika hilo na hawaamini kwamba lina sifa za kupewa jukumu hilo. Vyama vya upinzani nchini Angola vinalalamika pia kuwa kukabidhiwa shirika la Deloitte lenye makao yake nchini Uingereza, jukumu la kuandikisha wapiga kura kutawanyima wananchi wengi wa Angola haki yao ya kidemokrasia hasa kwa vile Angola katika miongo miwili iliyopita haijawahi kushuhudia mabadilishano ya kweli ya uongozi na hali imekuwa mbaya kiasi kwamba chama tawala cha MPLA kinahisi ndicho chenye hati miliki ya masuala yote ya Angola. Hofu nyingine waliyo nayo wapinzani nchini Angola ni kuwa, kama Rais Dos Santon atashinda katika uchaguzi ujao, basi atabakia madarakani kwa miaka 43 ambayo ni miaka mingi sana kwa nchi kuongozwa na mtu mmoja. Kiujumla ni kuwa licha ya manuva yote ya kisiasa yanayoweza kufanywa na chama tawala cha MPLA, lakini chama hicho na serikali ya Angola kiujumla, haiwezi kudharau mashinikizo ya wananchi hasa kwa kuzingatia kuwa, tarehe 19 mwezi huu wa Mei, maelfu ya wananchi wa Angola, waliitikia mwito wa chama cha upinzani cha UNITA wa kushiriki katika maandamano ya kupinga hatua ya serikali ya kumteua Suzana Inglês kuwa mkuu wa tume ya taifa ya uchaguzi.
No comments:
Post a Comment